Wananchi Mpanda waomba utekelezaji ahadi ya Makamu wa Rais

Katavi. Wananchi wa Kata ya Simulwa iliyopo Manisapaa ya Mpanda mkoani Katavi wamelalamikia kutotekelezwa kwa ahadi ya Makamu wa Rais aliyotoa Julai 22, 2022 kwa viongozi wa manisapaa hiyo ya ujenzi wa Barabara ya Mkumbo – Simulwa kwa kiwango cha lami.

Kwa takribani miaka miwili sasa, ujenzi wa barabara ya hiyo ambayo ni kero kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo, imeharibika na kwa muda mrefu imekuwa ikitatiza shughuli za usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, watumiaji wa barabara hiyo, wamesema kutojengwa kwa barabara hiyo na mamlaka za serikali za mitaa, ni kupuuza maelekezo ya Dk Mpango.

Dereva bodaboda na mkazi wa Simulwa, Paul Mtuwe (Kagusa) amesema barabara hiyo imekuwa kero kubwa kwa wakazi wa eneo hilo kwani inawakwamisha kufanya kazi zao kwa uhuru na hata usalama wao umekuwa mdogo nyakati za usiku kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Mtuwe amesema ujenzi wa barabara hiyo uliahidiwa na Makamu wa Rais, Dk Mpango alipokwenda kwenye kata hiyo kuzindua kituo cha afya cha Simulwa.

 Amesema tangu ahadi hiyo ilipotolewa, takribani miaka mitatu sasa, hakuna utekelezaji uliofanyika, huku wananchi wa maeneo hayo wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma kutokana na magari kushindwa kupita kuleta bidhaa katika eneo hilo.

“Tunataka kujua ahadi ya Makamu wa Rais aliyoitoa kwa viongozi wa Mkoa wa Katavi wakati amekuja kufungua kituo cha afya cha Simulwa mwaka 2022, imeipuuzwa ama ni nini kinaendelea? Tangu imetolewa ni miaka miwili sasa, alisema barabara hii itengenezwe lakini tunaona wako kimya,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Hao viongozi wa mkoa, wilaya mara nyingi wanapita huku, wanaona hali ilivyo lakini hawachukui hatua zozote, sasa tuseme ni kudharau ahadi ya kiongozi wa nchi aliyotoa mbele ya wananchi au nini?”

Kwa upande wake mwananchi wa kata hiyo, Jackson Machumbe, mkazi wa Simulwa, amesema ubovu wa barabara hiyo umesababisha nauli za bajaji na bodaboda kubanda, jambo ambalo linafanya maisha ya watu wanaotumia barabara hiyo kuwa magumu.

“Tunaomba watuletee vifusi kwenye hii barabara yetu ili wafukie haya mashimo yaliyojaa maji, tuwe tunapita wakati taratibu zingine zikiendelea kufanyika kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami,” amesema Machumbe.

Marysiana Mkungu, mkazi wa Simulwa amesema barabara hiyo imeharibika kutokana na kukosa mitaro, jambo ambalo linafanya maji kukosa uelekeo na kuharibu barabara kwani eneo hilo lina chemchem ambayo inatiririsha maji mwaka mzima.

“Tunaomba viongozi wa wilaya na mkoa waje watengeneze mitaro ili maji yawe na njia yake ya kupita na yasiharibu barabara kama ilivyoharibika hivi sasa,” amesema Mkungu.

Akizungumzia malalamiko hayo ya wananchi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli amekiri kuwepo kwa ubovu wa barabara hiyo, hata hivyo amesema hatua za ujenzi zimeanza na mkandarasi yuko kazini.

“Kweli malalamiko hayo tumeyapokea kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo lakini barabara ya Simulwa ipo kwenye mpango wa kujengwa Kwa kiwango cha lami hadi katika kituo chetu cha afya cha Simulwa. Kwa Sasa wataalamu wapo site wanachukua vipimo vya barabara hiyo ili kazi ya ujenzi ianze,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya watu watatakiwa kuhama ili kupisha ujenzi, hivyo amewatoa wasiwasi wananchi kwamba serikali yao ipo kazini na barabara hiyo itatengenezwa muda siyo mrefu, amewataka wawe wavumilivu katika kipindi hiki.

“Tumewaelekeza Tarura (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini) kumwaga vifusi na kuvisambaza maeneo korofi kwenye hiyo barabara ya Simulwa ili wananchi wapite kwa urahisi wakati taratibu zingine zikiendelea za ujenzi wa kiwango cha lami,” amesema Kumbuli.

Related Posts