CAG kutimua mbio kuikarabati Shycom

WAHITIMU waliosoma Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM) akiwemo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Charles Kichere wanatarajiwa kukimbia katika mbio za hisani maalumu kwa ajili ya kuchangia ukarabati wa miundombinu ya chuo hicho.

Mbio hizo zinazojulikana kama Shycom Alumni Marathon zitafanyika Septemba 21, mkoani Shinyanga na CAG akaweka bayana kwamba atakimbia mbio za Kilomita 21 (half marathon).

Akizungumza leo Alhamisi kwa niaba ya wahitimu wa chuo hicho, CAG Kichere amesema lengo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika ukarabati wa miundombinu kwenye sekta ya elimu.

“Kupitia mbio hizi za hisani kwa ajili ya kuchangia SHYCOM, tunaisaidia serikali kuboresha miundo mbinu kwa sababu, sisi tunatakiwa kuiunga mkono kwa kurejesha tunachokipata. Ni suala la hekima kujiunga kwa pamoja kurudisha hisani,” amesema.

Ametoa wito kwa wanafunzi wengine waliopita chuo hicho cha Shycom, kujitokeza kushiriki katika mbio hizo zitakazowezesha kupatikana kwa fedha za kukarabati miundombinu ya chuo hicho.
Pia amesema katika mbio hizo itakuwa ni nafasi nzuri ya wahitimu hao na jamii kwa ujumla kuungana pamoja kubadilishana mawazo na kuimarisha miili kupitia mazoezi.

Mratibu wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo, Arnold Bwechum amesema mbali na kuboresha miundombinu ya chuo hicho, mbio hizo zitaibua vipaji vya michezo, huku Mkuu wa Chuo hicho, Dk John Nandi amewapongeza wanafunzi hao kwa uamuzi wa kufikiria kukikarabati chuo walichosoma.

Dk Nandi amesema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo miundombinu ya njia ya kwenda kwenye mabweni na uhitaji wa viti-mwendo kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mbio hizo zilizoambatana na kauli mbiu isemayo: ‘kata upepo kwa afya kuiboresha Shycom’ huku washiriki watalazimika kulipa ada ya kiingilio cha Sh35,000 ambapo kiasi cha Sh30,000 kitakuwa kwa ajili ya vifaa vya michezo na Sh5,000 itaenda katika ujenzi wa miundo mbinu ya chuo hicho.

Related Posts