Kundemba yaishusha rasmi Ngome ZPL

USHINDI wa mabao 4-2 iliyopata Kundemba jana katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) umeishusha rasmi Ngome iliyokuwa ikicheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza ambayo sasa inazifuata Maendeleo na Jamhuri za Pemba zilizoshuka mapema.

Kundemba ambayo nayo haina uhakika wa kusalia kwenye ligi hiyo iwapo itachemsha katika mechi ya kufungia msimu, ilipata ushindi huo muhimu kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja na kuifanya ifikishe pointi 32 ikibaki nafasi ya 13 ikichungulia kaburi la kushuka daraja.

Kipigo hicho kinaifanya Ngome kusaliwa na pointi 27 na hata ikishinda mechi ya mwisho kufunga msimu haiwezi kuinusuru isishuke, kwani kanuni za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), timu nne za mwisho zinashuka daraja moja kwa moja na tayari Maendeleo na Jamhuri zimeshatangulia.

Ngome ina uwezo wa kufikisha pointi 30 zilizokwisha kupitwa na Kundemba, Hard Rock na New City zilinasubiria mechi za mwisho kujua hatma zao kwa msimu ujao wa ligi hiyo ambayo JKU inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 65 inahitaji pointi moja tu wikiendi kutangazwa bingwa.

Katika mechi hiyo ya jana jioni, Ngome ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia Paulo Godwin Ulomi aliyefunga dakika ya kwanza ya mchezo huo kabla ya Kundemba kusawazisha dakika ya tano baada ya Andulhimid Juma Abdi kukwamisha mpira kimiani.

Hata hivyo, Ngome ilicharuka tena na kuongeza bao la pili lililowekwa kimiani na Ulomi dakika ya 24 kabla ya Said Faki kuchomoa dakika sita baadae na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa sare ya mabao 2-2.

Kipindi cha pili Kundemba ilitumia vyema mabadiliko ya wachezaji iliyofanya kufunga mabao mengine mawili yaliyowapa ushindi huo kupitia kwa Hassan Abdalla dakika ya 83 na Mustafa Simai 90 na kuionyesha Ngome mlango wa kushuka daraja katika ligi hiyo inayofikia tamati wikiendi hii.

Katika mechi nyingine mbili zilizochezwa kisiwani Pemba, Maendeleo ilifumuliwa bao 1-0 na Uhamiaji katika mechi ya mapema saa 8 mchana na kuzidi kuboresha rekodi ya kuruhusu mabao mengi msimu huu ikifikisha mabao 69, huku saa 10 jioni, Hard Rock ilipata ushindi wa kushangaza mbele ya KVZ mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa FFU Finya.

Bao la Hard Rock liliwekwa dakika ya saba na Haruny Tumbwene Ndile, wakati lile lililoizamisha Maendeleo iliyokuwa ikicheza pia ZPL kwa msimu wa kwanza baada ya kupanda daraja lilitupiwa kambani na Yahya Haji Salmin dakika ya 88 na kuifanya Uhamiaji kufikisha pointi 44 na kujikita nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo.

Mechi za mwisho zitakazopigwa wikiendi hii ndizo zitakaotoa timu ya nne kushuka daraja moja kwa moja kuungana na Ngome, Maendeleo na Jamhuri, pia kutangaza bingwa mpya kazi ikiwa ni kwa JKU inayohitaji pointi moja tu, huku Zimamoto yenye pointi 62 ikiiombea timu hiyo mabaya na wenyewe washinde ili kufikisha pointi 65 na kubeba ubingwa kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa.

JKU imefunga mabao 44 na kufungwa 22, wakati Zimamoto imekwambia wavuni  mabao 51 na yenyewe kuruhusu 21.

Ubingwa wa Ligi hiyo hauna mwenyewe kwa sasa baada watetezi, KMKM iliyokuwa ikishikilia taji kwa misimu mitatu mfululizo kuchemsha mapema na kukosa pia tiketi ya michuano ya kimataifa kwa msimu ujao, kwao hata katika michuano ya Kombe la Shirikisho ilikwama na kwenda Chipukizi.

MSIMAMO WA LIGI KUU ZANZIBAR

20  Suleiman Mwalimu Abdallah (KVZ)

16 Ibrahim Hamad ‘Hilika’              (Zimamoto)

12  Ibrahim Isakah                           (KMKM)

10 Yazidu Idd Mangosogo             (New City)

    Arqam Ahmed Zubeir   (Kipanga)

9  Mudrik Abdi Shehe                      (JKU)

    Abdulhamid Juma Abdi               (Kundemba)

8  Omari Thani Abdalla    (Ngome/Malindi)

    Ramadhan Amri Mponda           (Malindi)

    Daud Goodluck Sovela               (Maendeleo)

New City vs Zimamoto    (Saa 10:30 jioni)

Jamhuri vs KVZ                  (Saa 10:30 jioni)

Malindi vs Kundemba       (Saa 10:30 jioni)

Mafunzo vs Ngome          (Saa 10:30 jioni)

Chipukizi vs Uhamiaji       (Saa 10:30 jioni)

Maendeleo vs Hard Rock (Saa 10:30 jioni)

KMKM vs Mlandege         (Saa 10:30 jioni)

Kipanga vs JKU                  (Saa 10:30 jioni)

Related Posts