Chalamila amkingia kifua DC ukamataji ‘makahaba’

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amemkingia kifua mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Hassan Bomboko juu ya mijadala inayoendelea ikikosoa operesheni aliyoifanya ya ukamataji ‘Dada Poa’, huku akisema haikuingilia faragha ya watu.

Mijadala hiyo iliibuka baada ya kuwapo kwa video mbalimbali ambazo zilionyesha namna operesheni hiyo ilivyokuwa ikifanyika usiku katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, huku akiambatana na waandishi wa habari.

Katika baadhi ya maeneo mkuu huyo wa wilaya aliingia katika baadhi ya nyumba za kulala wageni kutoa watu waliomo ndani jambo ambalo lilipingwa vikali.

Chalamila alipokuwa akihutubia katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee leo Alhamisi Juni 20, 2024 alijibu baadhi ya hoja zilizozungunzwa mitandaoni.

Amesema amepita katika mitandao ya kijamii na kuona lawama zikitolewa kwa kitendo kilichifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ya ukamataji ‘Dada Poa na Kaka Poa.’

Amesema kupitia mjadala huo baadhi ya kina mama wamelalamika wanawake kukamatwa na kuacha watoto nyumbani wakikosa uelekeo.

“Sasa kupitia siku hii ya mtoto wa Afrika naomba kwa uchache wa meneno na ukali mkubwa sana nifafanue yafuatayo. Katika mijadala ya watoto wameonyesha ni muhimu kupata malezi ya wazazi, ila ni fedheha kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika kutafsiri maisha ya kawaida kwa mama au baba kujiuza muda mwingi wa maisha na kusahau malezi ya watoto,” amesema Chalamila.

Amesema kilichofanyika kwa sasa ni kuanza kubadilisha mitazamo ya watu huku ndani ya halmashauri tayari zikianza kuandaa mpango maalumu wa kutoa mikopo itakayowasaidia wenye mawazo ya kuuza miili na kufanya vitendo ambavyo haviendani na tamaduni kuanza biashara ambazo zitasaidia watoto kuiga kutoka kwa wazazi.

Alionya vitendo vya kushabikia alichokiita ujinga ambao hayupo tayari kuuchekea, huku akizitaka taasisi zisizokuwa za kiserikali kutambua kuwa watoto waliopo hawana baba mwingine bali baba yao ni Afrika itakayowalea kuwa viongozi bora.

Amesema wanaohisi wamama wamedhalilishwa, amesema hawakudhalilishwa kwani hakuna aliyevuliwa nguo bali walijivua wenyewe.

“Hakuna hata mama mmoja aliyefanyiwa vitendo hivyo, bali wakichukuliwa kama walivyovaa wenyewe, wakiwa wamekaa hadharani kwa watu wenyewe na kupelekwa mahali ambapo ili isiwe aibu kwa watoto wanaokwenda shuleni alfajiri,” amesema Chalamila.

Amesema siku ya mkesha wa Eid mtoto wa miaka minne alilawitiwa nyumbani kwao akiwa peke yake baada ya wazazi kutoka huku mwingine wa miaka tisa akibakwa.

Amesema vyombo vya dola vinawafuatilia waliofanya vitendo hivyo, huku watoto wakifuatiliwa afya zao ili wawe sawa licha ya kuwa tayari wameathiriwa kisaikolojia.

“Stori hizi ukizisikiliza vizuri inatuamsha ari ya baba na mama kuwa wapenzi wakubwa wa melezi kwa watoto wetu na kamwe tusiwe mashabiki wa vitendo vinavyodhalilisha utu wa mwanamke, utu wa mtoto, au utu wa raia,” amesema Chalamila.

Amesema mtoto ni mtaji wa makuzi ya Taifa la baadaye, huku akisema kama katika biashara mtu anawekeza kwa ajili ya fahari ya uzee ni wakati wa kuwekeza kwa watoto kama fahari ya Taifa la baadaye.

Amesema hilo limfanye kila mtu kutokubali mtoto aharibiwe, atengwe, akosewe heshima, avunjiwe utu bali kufanya matendo mema na mazuri ambayo kila mtu atatamani kuiga matendo ya baba na mama.

“Baadhi ya watoto wa kidato cha kwanza na pili waliokamatwa katika maeneo wakiwa wanajiuza walisema wameiga tabia za mama zao na baba zao,” amesema Chalamila.

Alitumia nafasi hiyo kuwaambia wananchi kile walichokiona kupitia video mbalimbali za watu wakikamatwa ziwakumbushe Serikali hairidhishwi na mfumo huo ambao watu wanataka kuukubali kama tamaduni bali wanatafuta suluhisho.

“Kuwa ni vizuri basi chukua mkopo huu kidogo, fanya bishara kwa njia ya haki na halali itakayosaidia mwanao kuishi vizuri katika maisha ya baadaye, tukifanya hivi hakuna mtu atamjutia mwenzake bali kila mtu atafurahi kumuona mtoto wa jana amekuwa kiongozi mwema anayetumikia taifa lake,” amesema Chalamila.

“Huu ndiyo msimamo wangu ninapoongoza mkoa huu wa Dar es Salaam,” amesema.

Wakati yeye akiyasema hayo, alipozungumza na Mwananchi Jumanne wiki hii, Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Bomboko alifafanua jambo hilo huku akieleza haki zote zilifuatwa katika ukamataji ikiwemo kuwekwa huru kwa dhamana kwa waliokuwa wakihitaji.

“Wote waliokamatwa, dhamana ziliachwa wazi, wengine walipelekwa mahakamani wakakiri makosa wakaamrishwa kifungo au kulipa faini wengine walilipa faini wakaachiwa hakuna aliyekaa zaidi ya siku moja,” alisema.

“Zile kelele za kusema wengine wamelala chini, tumekamata watu 60 ni uongo kwa sababu idadi kubwa tuliyowahi kukamata ni 30 kule Sinza ambapo wanawake walikuwa 23 na wanaume 7,” alisema Bomboko.

Amesema ukamataji huo ulizingatia faragha za watu huku akihoji kuwa mtu aliyekaa utupu barabarani kujiuza ni faragha gani ambayo analinda.

Related Posts