Unguja. Uzalishaji wa karafuu umepungua kutoka tani 4,734.1 mwaka 2022 hadi kufikia tani 2,654.7 mwaka 2023 sawa na upungufu wa asilimia 43.9
Pia uzalishaji wa nazi umeshuka kutoka nazi milioni 119.747 mwaka 2022 hadi nazi milioni 79.807 mwaka 2023.
Hayo yamebainishwa leo Juni 20, 2024 na Waziri wa Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis wakati akijibu swali la mwakilishi wa Mwanakwerekwe Ameir Abdalla Ameir kwenye mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Zanzibar.
Mwakilishi huyo ametaka kujua tathmini ya sasa juu ya uzalishaji wa mazao ya biashara na upatikanaji wa fursa ya masoko kutokana na bidhaa wanazozalisha wakulima nchini.
Waziri Shamata amesema tathmini inaonyesha kwamba kwa mwaka 2023 kiwango cha uzalishaji wa nazi kimeshuka kutokana na kupungua kwa eneo la kilimo cha minazi kutoka ekari 22,000 hadi ekari 16,898.
Kutokana na hali hiyo, amesema uzalishaji wa zao hilo umepungua kutoka nazi milioni 119.747 hadi nazi milioni 79.807 na hilo limesababisha mahitaji na bei za nazi kuendelea kupanda. Kwa hivi sasa nazi nyingi zinaagizwa kutoka nje ya Zanzibar.
Kwa upande, amesema karafuu uzalishaji umepungua kutoka tani 4,734.1 mwaka 2022 hadi tani 2,654.7 mwaka 2023 sawa na upungufu wa asilimia 43.9.
“Hali hii imetokana na kuwa na msimu mdogo wa uzalishaji na mabadiliko ya tabianchi, hali iliyopelekea kukauka kwa mikarafuu mingi,” amesema
Wakati huohuo Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Shaaban Said Omar ameeleza mkakati wa Serikali katika kuishirikisha sekta binafsi kuliongezea thamani zao hilo,
Amesema wastani wa bei kwa tani moja ya karafuu kwa karafuu zinazozalishwa Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni Dola 8,500 za Marekani.
Amesema bei ya karafuu hubadilika kutokana na mahitaji ya soko yalivyo na hakuna bei maalumu ya karafuu za Zanzibar.
“Serikali kupitia Shirika la biashara (ZSTC) inaendelea na mpango wa kushirikiana na sekta binafsi kuliongezea thamani zao la karafuu na kwa kuanzia imeanza uzalishaji wa mafuta ya makonyo na mafuta mengine ya mimea, huku likiendelea kutafuta wawekezaji wengine kwa ajili ya kuliongezea thamani zaidi zao hilo,” amesema.
Wakati huohuo, Zanzibar imeweka mikakati mbalimbali ya kuendeleza uwekezaji wa bidhaa na huduma ili kuwezesha visiwa hivyo kupokea watalii wa daraja la juu.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema hatua hizo ni pamoja na kuwekeza katika kumbi za mikutano ya kimataifa, hoteli za daraja la juu hadi kwenye visiwa vidogo vidogo na kujikita zaidi katika utalii wa michezo.
Soraga amesema hayo akijibu swali la mwakilishi wa Mwanakwerekwe aliyetaka kujua jitihada zinazofanyika kuona Zanzibar inapokea watalii wa daraja la juu au la kwanza.
Pia Waziri Soraga amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazokua haraka katika kupokea meli za kitalii ambazo huingiza watalii wa daraja la juu.