Mkwamo wa bajeti watishia kuivunja serikali ya Ujerumani – DW – 20.06.2024

Chama cha Kansela Olaf Scholz cha Social Democratic, SPD, kile cha watetezi wa mazingira cha Kijani na chama cha Waliberali, FDP, vilivyoingia madarakani mwaka 2021, vina muda wa hadi Julai 3 ambayo ndiyo tarehe ya mwisho ya muhula wa sasa wa bunge kufikia muafaka.

Waziri wa Fedha Christian Lindner kutoka chama cha FDP ambaye ni muumini wa kubana matumizi, anataka kuwepo na akiba ya kiasi cha karibu euro bilioni 30, jambo ambalo vyama vya Kijani na SPD vimelikataa.

Soma pia: Je, ukomo wa deni la Ujerumani ni nini hasa?

Serikali hiyo ya muungano imekabiliana na mizozo mingi huko nyuma, lakini baadhi ya wadadisi wanaamini huu unaweza kuwa utakaosababisha kuvunjika kwa serikali.

Gazeti la Süddeutsche lilisema wiki hii kwamba mazungumzo yanayoendelea kati ya vyama washirika ndiyo yatakayoamua juu ya kuendelea kuwepo madarakani kwa muungano huo.

Wakati majadiliano ya bajeti yamekuwa magumu hata kabla, hayajawahi kudumu kwa muda mrefu kama hivi sasa.

Ujerumani, Berlin | Waziri wa fedha Christian Lindner
Waziri wa Fedha Christina Linder ambaye ni muumini wa kubana matumizi, anataka kuokoa kiasi cha euro bilioni 11 katika bajeti ya mwaka 2025.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance/dpa

Mtaalamu wa siasa za Ujerumani kutoka Taasisi ya Ufaransa inayojihusisha na masuala ya kimataifa na kimkakati, Jacques-Pierre Gougeon, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa mambo ni magumu kuliko kawaida.

Soma pia: Baraza la mawaziri Ujerumani lakutana kukwamua mkwamo

Aligusia hali ngumu inayotokana na utendaji duni wa Ujerumani katika nyakati za hivi karibuni, ambapo taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya likikabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei na kudorora kwa uzalishaji wa viwandani.

Kulingana na wizara ya fedha, mapato yatokanayo na kodi kwa mwaka 2025 yanatazamiwa kupungua kwa euro bilioni 11 kuliko ilivyokisiwa awali.

Hukumu ya mahakama ya juu nchini humo ya mwezi Novemba kwamba serikali hiyo ya muungano ilikuwa imekiuka sheria iliyowekwa kikatiba ya ukomo wa ukopaji wa mwaka, pia imepunguza nafasi ya matumizi mapya.

Soma pia: Rungu la Mahakama latikisa sehemu ya bajeti ya Ujerumani

Zaidi ya hayo, vyama vyote vitatu vinazidi kuwa na wasiwasi kuhusu viwango vyao vya uungwaji mkono baada ya kufanya vibaya katika uchaguzi wa mwezi huu wa bunge la Ulaya, ambapo kambi ya wahafidhina ya vyama vya CDU-CSU ilichukua nafasi ya kwanza, huku chama cha siasi kali za mrengo wa kulia cha AfD kikishika nafasi ya pili.

Kiini cha mkwamo kati ya FDP na washirika

Suala kuu linaloibua mvutano ni malipo kwa watu wasio na ajira. Waziri wa fedha Lindner anataka kupunguza malipo ya sasa, ambayo anaamini ni ghali mno na hayatoi motisha ya kutoka kwa watu kurejea kazini.

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Lakini chama cha SPD hakiwezi kukubaliana na hili, kwa sababu ahadi ya kuboresha malipo hayo ilikuwa ya kipaumbele katika kampeni ya chama hicho mwaka 2021, wakati wakitafuta kurejesha uungaji mkono wa wapiga kura wa kipato cha chini.

Soma pia: Scholz: Tutafanya juu chini kutatua mzozo wa bajeti

Pia kuna tofauti kuhusu hatua zozote zinazoathiri diplomasia na ulinzi, katika wakati ambapo Ujerumani inataka kusimamia maadili ya kiliberali ya Ulaya na kurekebisha jeshi lake linaloyumba kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Wakati wito umeongezeka kutaka sheria za madeni zilegezwe, Lindner na FDP wanakataa kabisa kushughulikia mabadiliko yoyote. Scholz, Lindner na Waziri wa Uchumi Robert Habeck, kutoka chama cha Kijani, wanatarajiwa kukutana Jumapili katika jaribio la kutatua mkwamo huo.

Chanzo: AFP

Related Posts