Beki mzawa Lameck Lawi amekuwa mchezaji wa kwanza kutambulishwa Simba SC katika kipindi hiki cha usajili wa kuelekea msimu mpya 2024/25.
Lawi ametambulishwa Msimbazi akitokea Coastal Union aliyoitumikia kwa juhudi kubwa msimu uliopita na kufanikiwa kuwa sehemu ya wachezaji walioipeleka klabu hiyo kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Taarifa iliyoandikwa kupitia SimbaAPP ambayo imeambatana na utambulisho wa mchezaji huyo imeeleza: Karibu Unyamani Lameck Lawi
Klabu ya Simba imefanikiwa kumsajili Mlinzi wa kati Lameck Elius Lawi kwa mkataba wa miaka mitatu kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja akitokea Coastal Union ya Tanga
Lawi ni kijana mwenye kipaji kikubwa na amekuwa ngome imara kwenye kikosi cha Coastal msimu uliopita na hicho ndicho kilichotuvutia kumsajili.
Usajili wa Lawi ni mkakati wa kuijenga Simba mpya yenye ushindani kuelekea msimu wa mashindano wa 2024/25.
Lawi mwenye umri wa miaka 18 na umbile refu anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa katika kikosi chetu kuelekea msimu mpya wa Ligi.
Lameck Lawi licha ya umri wake mdogo lakini ni Mlinzi mwenye uwezo mkubwa aliyewavutia wapenzi wa mpira nchini Tanzania na nje ya mipaka ya Nchi yetu na usajili wake tunategemea ataongeza kitu kikubwa katika kikosi akisaidiana na walinzi wazoefu waliokuwepo.