TIMU ya mpira ya kikapu ya Mchenga Stars iliifunga UDSM Outsiders kwa pointi 70-60, katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Spide.
Mchezo huo uliandaliwa na timu hizo kwa lengo la kuandaa timu zao katika mzunguko wa pili wa ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL) Julai 6.
Baada ya mchezo kumalizika kocha wa Mchenga, Mohamed Yusuph, alisema licha ya kushinda wapinzani wao walionyesha kiwango kizuri.
“Mchezo uliochezwa ulikuwa ni wa ufundi mkubwa kwa timu zote mbili,” alisema Yusuph.
Akizungumzia kuhusiana na timu yake, alisema imejipanga vizuri kuhakikisha inatinga hatua ya robo fainali.
Katika msimamo wa ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Mchenga Stars iko katika nafasi ya nne kwa pointi 27, huku nafasi ya kwanza ikishikwa na Dar City iliyo na pointi 29.