Waziri apokewa kwa mabango ya kudai maji Dar, atangaza mradi wa Sh18 bilioni

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza kujenga mradi wa maji wa Sh18 bilioni, wakazi wa Mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi, jijini Dar es Salaam wamegoma kuchimbiwa visima vya muda mfupi wakati wakisubiri mradi huo unaohusisha kutandaza mabomba na kujenga tenki la lita milioni sita.

Msingi wa kugomea kuchimbiwa visima na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ni kuchoshwa na ahadi za muda mrefu zinazotolewa.

Hayo yametokea leo Alhamisi, Juni 20, 2024 baada ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew kufika katika mtaani humo na kupokewa na mabango ya kulalamikia ukosefu wa majisafi.

Hatua hiyo ya Kundo kufika eneo hilo kujionea hali halisi, inakuja ikiwa ni siku tatu zimepita tangu Gazeti la Mwananchi lilipotoa habari maalumu ya adha ya maji kwa baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam ikiwaemo Mtaa wa Msumi ambao baadhi wanalazimika kutumia saruji ili kuyasafisha.

“Nimeyaona mabango, mmesema mmechoka kudanganywa masuala ya maji,” amesema Kundo wakati akisoma moja ya bango.

Kundo amesema ametumwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba Serikali imelenga kumtua ndoo mwanamke kichwani ili wasitembee umbali mrefu kutafuta maji.

“Wakati tunakuja tumesimamishwa Mshikamano wananchi wakasema wanataka maji, tukasimamishwa tena wakasema wanataka maji, nimekuja hapa nimepokewa na mabango, yakisema tumechoka kudanganywa,” amesema.

Amesema katika kushughulikia kero ya maji Mkoa wa Dar es Salaam, katika bajeti ya mwaka 2022/23 Serikali ilitenga bajeti ya Sh138 bilioni kwa ajili ya mkoa huo, lakini kwa kuwa fedha hizo hazikutosha Serikali ikaongeza bajeti ya Sh175 bilioni.

Amesema kwa Kata ya Mbezi pekee Serikali imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya kutandaza mabomba na Sh13 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa tenki na kuweka busta.

Hata hivyo, amesema mradi huo utalazimika kufuata taratibu zote za kihandisi.

“Ni lazima tukubaliane, mradi huu utakapoanza hauwezi kukamilika ndani ya mwaka mmoja, ni lazima uchukue muda. Sasa tunajiuliza je wananchi watafanyaje?

“Sasa tunafanyaje? Mpango wa muda mfupi, tumeamua Serikali wakati tunasubiri, hatutaruhusu watu waendelee kupata maji machafu. Sasa tunaelekeza mamlaka ya maji (Dawasa) wachimbe visima ili watu wapate maji,” amesema Kundo.

“Kibamba oyee, ukiwa hauna ugali unakunywa uji kwanza,” amesema Kundo.

Hata hivyo, kauli hiyo haikuwafurahisha wananchi na ndipo wakaanza kupiga kelele na Naibu Waziri huyo akawauliza:”Mnahitaji majisafi na salama?” Wakajibu,”ndioooo.”

Akauliza tena:”Tusubiri ule mradi wa Sh18 bilioni ukamilike baada ya mwaka mmoja au tutafute ufumbuzi wakati tunasubiri mradi wa Sh18 bilioni?”

Wananchi walijibu kuwa watasubiri. Walipoulizwa tena, wengine waliunga mkono na wengine walipinga.

Akizungumza baada ya kupewa nafasi, Desideria Diradina amesema wako tayari kusubiria mradi huo kuliko kuchimbiwa visima:”Maji ya chumvi tayari tunayo.”

Naye Joseph Kaduma amesema:”Kinachotusikitisha tunaambiwa kwamba huduma itapatikana labda baada ya mwaka mmoja, halafu mtuongezee visima. Kuna watu ambao walijiongeza wakachimba visima, tunalipa Sh4,000 kwa uniti moja, sasa mnataka mlete jinamizi lingine la kuchimbiwa visima, utakuwa ni mzigo mzito.”

Amesema kwa kuwa bomba la Dawasa lipo kilometa 10 kutoka Msumi, wavutiwe maji haraka:”Leo tunaambiwa tujengewe visima, litakuwa ni jinamizi kubwa.”

Aloyce Joseph amesema wataendelea kuusubiria mradi huo kwa kuwa wameshateseka na maji ya visima.

Awali, akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kingu Kiula amesema eneo hilo halina maji.

“Eneo hili la Msumi halina maji ya Dawasa kabisa. Lakini Serikali haijakaa kimya, tumefanya design ya mradi. Zimetegwa Sh13 bilioni na litajengwa tenki na kuweka busta,” amesema.

Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu amesema licha ya kero hiyo, Serikali ya awamu ya sita imejenga miradi ya maji.

“Changamoto iko hapa center ndio maana umekuja lakini mtendaji mkuu wa Dawasa ameshasema kuna mradi wa Sh13 bilioni,” amesema.

Related Posts