Moshi. Wakati mamia ya waombolezaji wakiaga mwili wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda (56), aliyefariki dunia kwa ajali ya gari yeye na dereva wake, serikali imetakiwa kuwabana madereva wote wakiwemo wa Serikali wanaovunja sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali zisizo za lazima.
Nzunda na dereva wake, Alphonce Edson(54) walifariki Juni 18, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea saa 8:30 mchana katika eneo la Njiapanda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye alikuwa akielekea Mkoani Arusha kikazi.
Nzunda ameagwa leo Juni 20, nyumbani kwake Shanty town, Manispaa ya Moshi na kusafirishwa jioni ya leo, kuelekea Goba, Mkoani Dar es Salaam kwa ndege ya Serikali ambapo kesho Ijumaa Juni 21, 2024, mwili huo utapelekwa Songwe kwa mazishi ambayo yatafanyika Jumamosi, Juni 22, 2024.
Viongozi wa dini wafunguka
Akizungumza katika ibada fupi ya kuaga mwili, Msaidizi wa Askofu na Wakili wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Padri Deogratius Matiika ameiomba Serikali kupitia vyombo husika vya usalama barabarani kuhakikisha madereva wanazingatia sheria zilizowekwa ili kupunguza majanga ya ajali ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu ambao ni muhimu kwa Taifa.
Padre Matiika amesema baadhi ya madereva wa Serikali wamekuwa wakizigeuza barabara kama ni za kwao peke yao bila kuchukua tahadhari wala kujali wasafiri wa vyombo vingine barabarani.
“Wengi wanaoendesha magari ya Serikali wamekuwa wakiendesha magari kwa spidi kubwa, jamani wahusika wajaribu kuliangalia jambo hili maana wanaingia barabarani bila tahadhari, nadhani vyombo vinavyohusika vihusike katika hili,” amesema Padri Matiika.
Ameongeza: “Wale ni kama vile barabara wanaona ni ya kwao peke yao, sizungumziii wale ambao wanakuwa kwenye misafara ya viongozi ni wale ambao unakuta hawako na viongozi lakini wanatembea kwa spidi kubwa, wakiwa kwenye shughuli zao za kawaida muda ambao siyo wa kazi.”
Amesema: “Dereva anafika barabarani anaona barabara ni ya kwake na spidi anayotembea nayo ni ya kwake, tunasikitika kwamba askari wetu hawa wa barabarani wanafanya kazi nzuri na kubwa lakini yanapopita magari haya yenye namba za serikali hawayasimamishi licha ya kwamba wanatembea kwa mwendo mkali.”
Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk Fredrick Shoo amesema Nzunda ambaye pia alikuwa mjumbe wa bodi ya Shirika la Msamaria Mwema la Hospitali ya Rufaa ya KCMC, alikuwa mtu muungwana, mtulivu na mcha Mungu ambaye aliheshimu watu.
“Wale wote tuliomfahamu Tixon Nzunda, alikuwa muungwana, mtulivu na mcha Mungu, tunamshukuru Mungu kwa ushuhuda wa maisha yake na uhusiano mzuri na watu wengine, sisi wana kilimanjaro tunawaheshimu viongozi wale wanaojiheshimu na kuwaheshimu watu kama Tixon alivyokiwa, Mungu atusaidie sisi tuliobaki tuendelee kuwaheshimu binadamu wenzetu, tutumike kwa uaminifu na tuendelee kumuheshimu Mungu,” amesema.
Ummy, Babu, wamlilia Nzunda
Akizungumza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Nzunda ameacha hadithi njema ambayo imeacha funzo kwa kila mmoja.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa kifo ndugu yangu Nzunda, sisi ambao tumefanya kazi naye tunaukumbuka uchapakazi wake, utiifu wake, umakini wake na utu wake kwa watu, kwenye hizi ofisi za umma tunajuana, hakika maisha ya Nzunda yameacha hadhithi njema.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ameelezea namna walivyofanya kazi na Nzunda akisema alikuwa wakifanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano mkubwa huku akieleza kuwa hajui kwa sasa atafanyaje.
“Alikuwa ni kiongozi mwadilifu lakini mtu mwenye msimamo, nitapata tabu sana, najiuliza maswali mengi, mafaili nitayapeleka wapi, maana yake likija faili kwangu nalipeleka kwa Nzunda, yeye akipata faili analileta kwangu likiwa limesheheni na wakati mwingine ameshauri nini tufanye, kwa hiyo kazi yangu ilikuwa rahisi sana, nafikiria leo tutafanyeje,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema Nzunda alikuwa mtu mwenye misimamo na kiongozi ambaye hakunyanyua mabega katika uongozi wake.
“Kwa muda mfupi tuliokaa na Nzunda na kufanya nae kazi, Kilimanjaro, alikuwa shujaa, hakuwahi kunyanyua mabega, Mungu alimgawia tunu nyingi na alijitahidi kuzigawa kwa kila aliyehitaji ushauri,” amesema.
Ameongeza kuwa “Alikuwa mtu mwenye misimamo asiyeyumbishwa, na tuliokuja hapa tumejifunza unapopata nafasi ya utumishi, fanya kazi yako kwa uaminifu na uadilifu ili wengine wavune kwako”.
Katibu tawala (Ras) Mkoa wa Arusha, Missile Mussa, amesema siku ya tukio waliwasiliana kwa ajili ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (Kia), yeye akitokea Arusha na Nzunda akitokea mkoani Kilimanjaro, lakini alipofika eneo la King’ori alipata taarifa ya ajali.
“Makatibu tawala tumepokea msiba huu kwa huzuni kubwa, tumekuwa na ushirikiano mkubwa, hakika alikuwa mshauri mzuri, msikivu na muadilifu,” ameeleza.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe amemuelezea Nzunda kuwa alikuwa akiongozi aliyehusika na maisha ya watu na kwamba katika utendaji wake wa kazi hakuwa mrasimu.
“Alikuwa kiongozi na mtumishi aliyehusika na maisha ya watu, sisi wabunge wa Kilimanjaro tunajivunia mambo mengi, ni kiongozi ambaye hakuwa mrasimu na hili ni somo letu sote, ni mtu aliyekuwa akitafuta majawabu, ni mtu ambaye alikuwa akisukuma hatua ziende mbele.”
“Siyo kawaida sana kumpata mtu wa namna hii kwenye utumishi wa umma, kwetu sisi ni somo kwa wale waliobaki ofisini, tunaweza kumuenzi kwa kuhakikisha tunapunguza urasimu, tunatoa majibu na kuwa sehemu ya kusukuma hatua mambo yakwenda kutokea,” amesema.
Familia yaishukuru Serikali
Akitoa neno la Shukrani mmoja wa wanafamilia, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ndege ya kusafirisha mwili wa mpendwa wao kutoka Moshi hadi Dar es Salaam na kisha kuupeleka Songwe.
Pia, amemshukuru Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwa namna alivyowakimbilia na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanharo, Nurdin Babu kwa namna alivyoubeba msiba huo.