Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku saba kabla ya kuanza kwa maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), kampuni za ndani 2,979 zimethibitisha ushiriki wake hadi sasa huku maandalizi yakifikia asilimia 79.
Pia, tofauti na miaka mingine, mwaka huu wananchi watakuwa na uwezo wa kukata tiketi kupitia mitandao ya simu badala ya kutegemea madirisha pekee, jambo ambalo linatarajiwa kupunguza msongamano.
Mwananchi Digital imefika katika viwanja wa Julius Nyerere maarufu Sabasaba, Dar es Salaam leo Alhamisi Juni 20, 2024 kushuhudia maandalizi mbalimbali, zikiwemo shughuli za ujenzi wa mabanda ya muda, upakaji rangi na usafi.
Maandalizi hayo yamekuwa ni fursa ya ajira kwa watu mbalimbali wakiwemo wanawake waliochangamkia fursa za usafi na upambaji ndani ya viwanja hivyo.
Kwa mujibu wa ratiba, maonyesho hayo yataanza Juni 28 hadi Julai 13, 2024 na kampuni za nje zilizothibitisha ushiriki wake zimefikia 223.
Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja wa mafundi, Juma Hussein waliokutwa wakifanya maandalizi kwenye moja ya banda, amesema msimu huu ni wa neema kwao.
“Unajua wengine wanakuja humu wakijua mafundi watawakuta, akiona umetengeneza vizuri anakwambia basi ukimaliza uhamie na kwangu, ndiyo tunavyopata fedha. Tangu Jumatatu tuko humu,” amesema Hussein.
Zainab Athuman ambaye amekutwa akijiandaa kupamba moja ya mabanda amesema kwa miaka mitatu sasa amekuwa mnufaika wa maonyesho hayo na kila yanapofanyika idadi ya wateja inaongezeka.
“Watu wanaambiana, ukiwa mwaminifu unapata hela, kwa sababu mwingine muda wa kukusimamia hana, anataka akikupa fedha akute kazi imefanyika, ukimfanyia kazi vizuri haoni shida kukuuganisha na wengine,” amesema Zainab.
Baadhi ya mama lishe wameanza kunufaika na fursa za biashara kwa kuuzia watu wanaofanya maandalizi ndani ya viwanja hivyo.
“Sisi sehemu yenye watu ni mtaji wa biashara, tumeanza kidogo kidogo na tutaendelea hadi siku ya mwisho ya maonyesho,” amesema mmoja wa mama lishe.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis mbali na waliothibitisha kushiriki, maonyesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee ukilinganisha na miaka nyuma kwani wananchi wataweza kukata tiketi kwa njia ya mitandao ya simu.
Pia amesema kutakuwa na milango ya kielektroniki ambapo wananchi na magari mengine yataweza kuingia na kupunguza usumbufu na msongamano.
Mpaka sasa nchi 25 zimethibitishwa kushiriki, kampuni za nje 223 na washiriki wa ndani 2,979.
“Haya ni mafanikio makubwa kwa sababu siku bado lakini kampuni nyingi tayari zimethibitisha na hii haijawa kwa bahati mbaya, kwani Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisafiri nchi mbalimbali kuitangaza Tanzania, haya ni matokeo,” amesema Latifa.
Amesema maonyesho hayo ni moja ya njia ya kuchochea uchumi wa nchi kwani yanachechemua shughuli mbalimbali ikiwemo za usafirishaji, malazi na hata ajira za muda mfupi kwa baadhi ya watu.
Miongoni mwa yatakayofanyika katika maonyesho hayo ni maadhimisho ya siku za mataifa saba zitazofanyika kwa siku tofauti tofauti.
“Kutakuwa na Siku ya Taifa ya China, Misiri, Russia, India, Japan, Korea na nyingine. Pia kutakuwa na onyesho la roboti ambazo tayari zimeshaingia na ziko kwenye majaribio,” amesema Latifa.