Tari wathibitisha ‘chia seeds’ kutibu mifumo ya uzazi kwa wanawake

Mbeya/Dar. Wakati mmea wa ‘chia seeds’ maarufu kivumbasi, ukitumiwa na baadhi ya watu kupunguza unene, utafiti mpya umeonyesha zina uwezo wa kutibu mifumo ya uzazi, ikiwemo kuongeza ute sehemu za siri za mwanamke.

Utafiti huo uliofanyika kwa miaka 10, umeleta matokeo chanya kwani licha ya kutibu mifumo ya uzazi, pia umethibitisha kuwa na uwezo wa kupunguza uzito mkubwa ‘unene’.

Utafiti huo uliofanywa kupitia Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Uyole kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti Tari, ulilenga kutafuta suluhu la changamoto ya jamii kukabiliwa na tatizo la uzito mkubwa na mifumo ya uzazi.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi June 20 2024 na Mwezeshaji wa chuo hicho cha mafunzo, Richard Msuya wakati wa maonyesho ya shamba darasa la kilimo-biashara mikoa ya nyanda za juu kusini, lililoshirikisha   wadau wa Shirika la kimataifa la Care Tanzania.

Amesema sababu za mmea huo kuongeza ute kwenye uke mkavu wa mwanamke ni kutokana na virutubisho vya mbegu zake vinavyopatikana, baada ya kuloweka kwenye maji na kuteleza hivyo mtumiaji akinywa hufanya kazi haraka ya kuzalisha ute uliopotea.

Walipotakiwa kuzungumzia hilo, wataalamu wa afya ya uzazi na homoni, wamesema mbegu hizo zina faida nyingi kiafya, ingawaje bado hakuna tafiti za moja kwa moja ambazo wamewahi kuzifanya.

“Zina faida nyingi kiafya na wengi wamekuwa wakizitumia ingawaje zisijawahi kuzichambua vizuri, ni kama ilivyo kwa mmea wa alovera,” amesema Daktari Bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Kishiriki  Muhimbili (Muhas), Fredrick Mashili.

Alipoulizwa sababu za ute kukauka kwa mwanamke, ametaja kitu cha kwanza kuwa ni homoni.

“Homoni ni sababu kuu ukiachana na zile zingine za kukoma kwa hedhi. Lakini mambo mengi ni saikiolojia na mhemko zaidi. Saikolojia vinaingiliana na mfumo wa homoni na zinachangia katika utengenezaji wa ute wa mwanamke ukiachilia mbali umri,” amesema Dk Mashili.

Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na kina mama, Abdul Mkeyenge amesema ufanyaji wa tendo la ndoa kuna kuandaana hatua ambayo mwili wa binadamu hutoa matokeo ‘ute’ kuashiria sasa mwanamke amekuwa tayari.

“Sehemu za siri za kike zimeundwa maalumu na vilainishi vyake vya kiasili na visivyo na madhara. Kuna majimaji fulani huwa yanatoka yenye asili ya kuteleza au ute yale ndiyo yanasababisha unapokutana na mwenza wako usipate michubuko,” amesema.

Amesema kibaolojia mwili hujiandaa wenyewe na ni lazima kabla wote wawe tayari kiakili na kifikra.

Hata hivyo amesema wapo wengine hata wakiandaliwa huwa wanakuwa wakavu kutokana na aina ya magonjwa au kuwa na upungufu wa baadhi ya vichocheo hali ambayo husababisha sehemu za siri kuwa kavu, “Mtu kama huyu anatakiwa kufika kwenye vituo vya afya ashauriwe na wataalamu baada ya kufanyiwa vipimo.”

Kufuatia hilo, wakulima mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kugeukia kilimo cha zao hilo uliofanyiwa tafiti na kubainika kutibu mifumo ya uzazi, uzito mkubwa sambamba na kuongeza ute sehemu za siri.

Msuya amesema tafiti zilizofanywa na kituo hicho zimezaa matunda na kuleta matokeo chanya hali iliyosababisha msukumo mkubwa kwa jamii kuchangamkia tiba hiyo.

“Soko lake kwa mikoa nyanda za juu kusini na kaskazini lilo juu na wenzetu nchi zingine walitangulia kulima zaidi mmea huu, kutokana na mahitaji kuwa makubwa tunatoa hamasa kwa wakulima kujikita katika uzalishaji,” amesema.

Msuya amesema kwa mwaka wastani wa tani 10 huzalishwa na mikakati ya sasa ni kufikia tani 100 ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

“Tunapima mahitaji kulingana na soko lilivyo, unaweza kukuta mtu leo kanunua kilo kumi kesho kilo hamsini huku kilo moja inauzwa Sh20,000 mpaka Sh25,000,” amesema.

“Hili ni zao la asili ambalo lina miujiza mikubwa katika tiba mbalimbali za maradhi yanayo changiwa na mifumo ya vyakula na unywaji wa pombe kupita kiasi,” amesema.

Msuya ametumia fursa hiyo kutaka jamii kuachana na ulaji mkubwa wa nyama na matumizi ya pombe kupita kiasi ili kukabiliana na madhara yanayoweza kuzuilika.

“Kuna watu wanaona fahari kula nyama nyekundu ya kitimoto au mbuzi lakini kiafya kiasi kikubwa inaenda kutengeneza sumu mwilini,” amesema.

Mkurugenzi wa Shirika la Care Tanzania, Prudence Masoko amesema kwa kushirikiana na serikali  wamewekeza kufanya mabadiliko katika sekta ya kilimo katika suala la tafiti kwa kipindi cha miaka mitano.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 17 zilizonufaika na mradi wa shamba darasa na kilimo biashara huku kwa mikoa ya nyanda za juu kusini wilaya ya Iringa imenufaika.

Meneja mwandamizi wa rasilimali wa Care Tanzania, Christian John amesema wamejikita kufanya tafiti mbalimbali katika sekta ya kilimo kwa kuhusisha taasisi za serikali, kupitia Wizara ya Kilimo kwa kutumia mbinu za ugani za tafiti za hatua za uzalishaji na uhakika wa masoko.

Wataalamu walieleza kuwa kukosa ute wakati wa tendo la ndoa ni dalili ya kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni ya estrogen kuliko progesterone ila kuna dalili nyingine ambazo zinaweza kutokea kwa sababu ya kukosa ute ikiwemo;

1.       Kukosa hisia na hamu ya tendo

2.       Kuhisi maumivu wakati wa tendo

3.       Uwepo wa damu baada ya tendo

4.       Hedhi kukosa mpangilio maalumu

5.       Matumizi ya uzazi wa mpango na vidonge vya P2, vitanzi, sindano

Related Posts