YANGA inapiga hesabu kuwaficha mastaa wake Urusi kujiandaa na msimu mpya wa kimashindano, lakini iwapo itakwama kabisa basi itatua Sauzi na ikakutana uso kwa uso na kocha wa zamani wa timu hiyo, Nasredine Nabi.
Hesabu za kwanza kwa Yanga ni kwenda Urusi kujichimbia kwa maandalizi ikiwa na mualiko wa klabu rafiki ya CSKA Moscow na Mwanaspoti linafahamu pia mezani kwa mabosi wa klabu hiyo kuna ofa ya maana nyingine.
Kama Yanga haitakwenda Urusi basi nafasi kubwa itaenda Afrika Kusini ambapo klabu ya Kaizer Chiefs imeipa mualiko wa kucheza nao mchezo mmoja wa kirafiki wa kimataifa.
Kaizer Chiefs inataka kucheza mechi moja na Yanga iliyoandaliwa na kampuni ya magari ya Toyota, lakini Yanga inataka pia kama itakubali mualiko huo ikaweke pia kambi huko baada ya msimu uliopita kuwaalika Wasauzi na kucheza nao katika mechi ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi.
“Unajua tuliwaalika wenzetu hapa msimu huu mwanzoni na wao wametutaka kwenda huko kuna mechi pale ilyoandaliwa na Toyota, sasa sisi tunatakiwa na wanasisitiza sana tuende,” alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga na kuongeza;
“Kama tukiona Ulaya ni vigumu kwenda sasa basi tunaweza kwenda hapa Afrika Kusini, ili tucheze hiyo mechi lakini haya yote tutaamua ndani ya wiki moja kutoka sasa.”
Endapo Yanga itakwenda Afrika Kusini kuna uwezekano mkubwa kwa timu hiyo, kukutana na kocha Nabi, aliyewahi kuinoa timu hiyo na kuipa mataji sita tofauti, yakiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili ya Ngao ya Jamii na mengine kama hayo ya Kombe la Shirikisho mbali na kuifikisha timu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria waliofungana nao mabao 2-2, Yanga ikilala nyumbani 2-1 na kushinda 1-0 ugenini.
Kaizer Chiefs imeshamaliza na Nabi baada ya kumtuma mmoja wa mabosi wake kwenda nchini Morocco kumalizana na kocha huyo,zoezi ambalo lilifanikiwa.
Nabi anataka kuachana na klabu yake ya Sasa ya FAR Rabat, ambayo imekosa ubingwa kwa dakika za mwisho ukitua kwa mahasimu wao Raja Athletic, hatua ambayo imemkera kocha huyo Mtunisia na anataka msimu huu ukimalizika aondoke fasta.