Wanyeche avunjwa ukimya, aitaja Lugalo

MSHINDI wa mashindano ya Gofu ya Alliance, yaliyofanyika wikiendi iliyopita mjini Morogoro, Enoshi Wanyeche ameweka wazi yeye ni mchezaji wa klabu ya Gofu ya Lugalo na sio Kili Golf ya Arusha kama alivyoripotiwa katika matoleo mawili ya gazeti hili.

Akizungumza na Mwanaspoti jana asubuhi, nyota huyo alisema ni kweli amekuwa akifanya mazoezi na kuwepo mara kwa mara Kili Golf, lakini hiyo haina maana ni mchezaji wa klabu hiyo, ila yeye ni mchezaji wa Lugalo.

“Nadhani aliyenukuliwa alichanganya, ni kweli mara kwa mara nimekuwa nikifanya mazoezi na Kili Golf, lakini haina maana mie ni mchezaji wa klabu hiyo. Mie nipo Lugalo na hata katika mashindano hayo ya Morogoro nilienda kama mchezaji wa klabu ya Gofu ya Lugalo,” alisema Wanyeche.

Katika habari za awali zilizotoka katika magazeti mawili tofauti yalimnukuu nahodha wa klabu ya Morogoro Gymkhana, Seif Mcharo akimtaja Wanyeche kama mchezaji wa Kili ya Arusha aliyefunika katika mashindano ya Morogoro yaliyosimama siku ya kwanza akiongoza ikichezwa mashimo 17.

Hata hivyo, hadi mwisho ya mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku tatu, Wanyeche alizamisha mipira katika mashimo 54 kwa jumla ya mikwaju 225 na kuibuka kidedea, huku Michael Massawe alikuwa wa pili, ilihali wachezaji watatu Seif Mcharo, Isihaka Daudi na Julius Mwizani wakifungana nafasi ya tatu kwa kila mmoja kupata mikwaju 233, japo kwa sheria ya gofu ya kuhesabu kutoka mwisho (countback), Mwizani ni wa tatu, Mcharo wa nne na Daudi alimaliza na tano.

Related Posts