Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka maofisa habari wa Serikali kutumia ujuzi walioupata katika kikao kazi cha siku mbili ili kuboresha utendaji kazi wao na katika kufanikisha hilo, Serikali itawapatia vitendea kazi.
Katika kikao kazi hicho cha 19 kilichoanza jana Juni 20 na kutamatika leo Juni 21, 2024, mapendekezo manne yatakayoongeza ufanisi wa utendaji kazi wao yametolewa.
Mapendekezo hayo yaliyowasilishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba ni ukamilishaji wa ujenzi wa mifumo ya Tehama kuanzia mwaka wa fedha wa 2024/25, kuongeza kasi ya utoaji taarifa kwa jamii, kuratibu mafunzo kila wakati na kikao kazi kijacho kifanyike Zanzibar.
Akizungumza wakati akifunga kikao kazi hicho, Waziri Nape amesema ujuzi huo utakuwa na maana endapo mabadiliko yataonekana katika utendaji kazi wao na wamekubaliana mafunzo ya kikao kazi yawe yanafanyika kila mwezi.
“Nimemuagiza Mkurugenzi wa Habari Maelezo atengeneze utaratibu wa kuendesha mafunzo haya kwenye kanda zenu kila mwezi na awe na ratiba ya mahali fulani ili tuendelee nayo hata kama mada moja moja,” amesema.
Amesema mafunzo yanaweza kuwaongezea uwezo na thamani kwenye maeneo yao ya kazi na hasa katika zama hizi za matumizi ya mitandao na Tehama kwa ujumla.
Pia, amesema kazi za maofisa habari hao si tu kutoa taarifa za Serikali na taasisi kwa umma lakini wana wajibu wa kupeleka taarifa zinazoendelea kutoka kwenye jamii wanazozihudumia.
“Tusiwe maofisa habari wa kupeleka taarifa kwa umma peke yake, bali tuwe tunachukua taarifa za umma kupeleka kwenye taasisi zetu na kuzishauri namna ya kuboresha huduma zetu,” amesema.
Nape amesema kazi ya maofisa hao ni kujenga mitazamo kwa jamii juu ya mambo mbalimbali yaliyofanywa na Serikali pamoja na taasisi wanazohudumu.
Amesema kufanya hivyo itafanya jamii kuwa na taarifa zitakazowawezesha kufanya uamuzi sahihi kwa maendeleo yao, hivyo wana nguvu zaidi ya hiyo ya kupashana habari.
Katika kujenga taasisi ili zisisemwe vibaya, amesema hawatakiwi kufunika mambo wakati wakisemwa vibaya na huo ni wajibu wa ofisa habari kuifanya taasisi yake isipakwe matope.
Akipokea maagizo hayo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Matoba amesema kwake ni bahati kwa kukutana na watendaji wote na kupata maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa Rais.
“Najiona mtu mwenye bahati sana kuwa na Waziri anayesisitiza kuishi, pia nimeteuliwa Jumamosi usiku na siku inayofuata nilikuwa hapa na hii ni kazi yangu ya kwanza tangu nimeripoti,” amesema.
Hivyo, amesema hayupo tayari kumuangusha waziri na mtangulizi wake aliyepita pamoja na maofisa waliofika katika kikao kazi hicho.