Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji na Shirika la Reli Tanzania (TRC) yanatoa fursa kwa shirika kwa hilo kusafirisha washiriki wa mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka jijini Dar es Salaam hadi Dodoma na kurudi kwa kutumia treni ya kisasa ya mwendokasi (SGR) ya shirika hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Kupitia makubaliano hayo inatarajiwa kuwa washiriki zaidi ya 1,000 wa mbio hizo kutoka jijini Dar es Salaam watatumia usafiri huo wa haraka na wa kisasa zaidi ili kushiriki mbio hizo zitakazofanyika tarehe 28 Julai mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri wa jijijni Dodoma.
Lengo kuu la mbio hizo ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika mapema leo Ijumaa kwenye ofisi za TRC jijini Dar es Salaam ikihusisha viongozi waandamizi na maofisa wa pande zote mbili ambapo ilishuhudiwa Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Waziri Barnabas wakisaini makubaliano hayo kwa niaba ya taasisi zao.
Hafla hiyo ilitanguliwa na safari ya wadau hao kutoka jijini Dar es Salaam hadi Morogoro na kurudi hatua ambayo kutoa fursa kwa maofisa wa benki ya NBC na wadau wengine wakiwemo baadhi ya wakimbiaji kutoka vilabu mbalimbali vya wakimbiaji jijini Dar es Salaam kuweza kupata uzoefu wa usafiri huo kabla ya safari hiyo inayotarajiwa kufanyika siku moja kabla mbio.
“Ushirikiano huu pamoja na kutoa fursa kwa washiriki wa mbio zetu kutoka jijini Dar es Salaam na Morogoro kwenda jijini Dodoma, pia unalenga kuthibitisha dhamira yetu kama taasisi katika kuunga mkono jitihada kubwa zilizofanywa na serikali hadi kufanikisha mradi huu mkubwa na wa kisasa.’’
“Ili kujijengea uzoefu na kuwa mashuhuda kwa washiriki wa mbio zetu watakaotumia usafiri huu siku chache zijazo, sisi kama benki na wadau wetu wengine wakiwemo wadhamini tumetumia usafiri huu leo ili kujionea ubora wake ambao kiukweli umetuvutia sana…pongezi kubwa kwa serikali na TRC kwa hatua hii muhimu,’’ alisema Waziri.
Kwa mujibu wa Waziri matumizi ya treni hiyo yatatoa fursa ya chaguzi zaidi za aina ya usafiri kwa washiriki wa mbio hizo kutoka jijini Dar es Salaam kwa kuwa wapo washiriki wengine ambao watatumia aina nyingine za usafiri ikiwemo mabasi, magari binafsi na ndege.
“Pamoja na aina nyingine za usafiri washiriki watakaopata fursa ya kutumia treni hii ya SGR watahakikishiwa burudani mbalimbali mwanzo hadi mwisho wa safari wakiwa kwenye mabewa yatakayoandaliwa mahususi kwa ajili yao,’’ aliongeza.
Aidha, Waziri aliwashukuru wadau mbalimbali yakiwemo mashirika na kampuni mbali mbali wakiwemo Sanlam Insurance ambao ni wafadhili wakuu wa mbio hizo huku wadau wengine wakiwa ni Jubilee Allianz General Insurance, Wasafi Media, Garda World, Metropolitan, SGA,SBC, Benki za CRDB na NMB, Computech Solutions na Hans-Paul.
Awali akizungumza kwenye tukio hilo, Bw Kadogosa alisema ushiriki wa shirika hilo kwenye mbio hizo unalenga kuunga mkono agenda ya kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wanaosomea taaluma ya ukunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto. Aidha aliwahakikishia washiriki wa mbio hizo kupata huduma na uzoefu wa kipekee hasa kutokana na ukweli kwamba safari hiyo itakuwa ni miongoni mwa safari za mwanzo za treni hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
“Ni matumaini yangu kwamba washiriki wa mbio hizi watapata uzoefu wa safari ambao hawajawahi kuupata kabla kutokana na ukweli kwamba safari hii itakuwa miongoni mwa safari zetu za awali kabisa kati ya Dar es Salaam na Dodoma. Washiriki watapelekwa Dodoma na watarudishwa wakiwa na furaha zote hivyo nawasisitiza sana wakazi wa Dar es Salaam na Morogoro wajisajiri kwa wingi kwa ajili ya kushiriki mbio hizi kwa kuwa umbali kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma sio changamoto tena kupitia treni hii,’’ alisema Bw Kadogosa.
Akizungumzia ushiriki wa mbio hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Bi. Tasiana Masimba alisema washiriki wanaweza kujisajili kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz na kuchangia kiasi cha TZS 35,000 kwa usajili wa washiriki mmoja mmoja au 25,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu wanaozidi 25.