KAMA kuna hadithi tamu ya kuisimilia katika ulimwengu wa soka, basi ni hii ya muujiza wa kocha Xabi Alonso na klabu yake ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
Baada ya miaka 120 ya uhai wao, Bayer Leverkusen wameshinda kwa mara ya kwanza taji la Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga).
Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1904 ilikuwa imeshinda mataji mawili tu kabla ya hilo la Ligi Kuu msimu huu.
Mataji hayo ni Kombe la UEFA ambalo sasa limerithiwa na Europa League (1987/88) na DfB Pokal (sawa na Kombe la FA) ambalo walishinda msimu wa 1992/93.
Lakini msimu huu, wako kwenye mwelekeo wa kushinda mataji matatu, miujiza iliyoje hii? Ligi Kuu tayari ipo kibindoni. Kwenye DfB Pokal wako fainali na watacheza na FC Kaiserslautern, Mei 25, 2024.
Halafu Ulaya wapo robo fainali ya Europa League na wameshashinda mchezo wa mkondo wa kwanza 2-0 dhidi ya West Ham United ya England. Haya yote yanafanyika katika kipindi ambacho timu hiyo inacheza tu mechi zake bila kupoteza.
Hadi wanatawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Ujerumani kwa ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Werder Bremen, Bayer Leverkusern wameweka rekodi ya taifa hilo kucheza mechi nyingi zaidi bila kupoteza.
Wamecheza mechi 43 katika mashi-ndano yote bila kupoteza hata moja. Rekodi hii ndiyo imewafanya wamba hao kubatizwa jina la utani la NEVERLOSING yaani timu ya kutopoteza, likitumika jina lao la asılı kuchagizia.
Hata hivyo, jina hili ni kama linarekebisha kile kilichotokea miaka zaidi ya 20 iliyopita.
Ilikuwa msimu wa 2001/02 wakiwa chini ya kocha Klaas Topmoller, Leverkusen walikuwa kwenye uelekeo wa kushinda mataji matatu hadi siku 11 kabla ya msimu kwisha.
Ikiwa na kikosi cha dhahabu cha kina Dimitar Berbatov, Lucio, Ze Bebeto, Michael Balack na wengineo wengi wakali kilijikuta kikishindwa kuandika historia dakika za mwisho kabisa.
Kwenye ligi walibaki na michezo mitatu na walitakiwa kupata alama nne tu katika mechi hizo, lakini zikawapalia, wakaukosa ubingwa. Wakapoteza mechi kimaajabu na ubingwa ukaenda kwa Borusia Dortmund.
Wiki moja baadaye wakacheza na Shalke 04 kwenye fainali ya DfB Pokal na kufungwa mabao 4-2. Baada ya kupoteza mataji hayo mawili likabaki taji moja – nalo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mbele yao walikuwepo Real Madrid na Leverkusen wakapoteza tena fainali. Ndani ya siku 11 wakapoteza kila taji muhimu walilowania.
Kitlendi cha kupoteza mechi hizi kiliwafanya waandishi wa habari waichagulie timu hiyo jina jingine litakalofanana na tabia waliyoionyesha. Ndipo ikaanza kuitwa NEVERKUSEN yaani hakuna kushinda taji.
Lakini miaka mingi baadaye hatimaye wameshinda Ligi Kuu na kufanya kile ambacho kimekuwa kikiwakwaza miaka yote. Watu wameshasahau kama walishawahi kuipa majina ya ajabu Leverkusen kwa sababu ya hizi rekodi bora za msimu huu. Xabi Alonso amebadisha kila kitu kwenye mechi za Leverkusen akicheza kwa kushambulia sana. Mwisho wa siku, ubingwa ni maji na ni kama umewafikia mikononi.