Tanzania yaanza kutekeleza makubaliano ya AU ya utunzaji mazingira

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeweka mkakati wa kupanda hekta milioni 5.2 za miti na kulinda misitu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika (AU) ya utunzaji misitu na ardhi.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi za kuokoa hekta milioni 100 za misitu barani Afrika kufikia mwaka 2030, ulioahidiwa na nchi 34 za Afrika mwaka 2015.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, amesema Tanzania imefanikiwa kupanda hekta milioni 2.4, sawa na asilimia 46 ya lengo lake.

Akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa nane wa AFR100 ulioandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya AUDA-NEPAD na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Waziri Kairuki amebainisha umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa miti katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Kairuki amesema, “Misitu ilikuwa imeteketea kutokana na matumizi ya mkaa, mbao, na magendo, hivyo Afrika tukakubaliana kuokoa hekta milioni 100 na nchi 34 zikatoa ahadi ya kutekeleza hilo.”

 Ameongeza kuwa, ili kufanikisha mpango huu, Tanzania imeweka mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kwa mifumo ya kielektroniki.

“Miti hii lazima ipandwe, ilelewe, ikue ili tupate manufaa yake, hivyo lazima tufuatilie upatikanaji wa taarifa na ripoti katika mpango huu,” amesisitiza.

Kamishna wa uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, amesema dunia ilipanga kuokoa hekta milioni 350 za ardhi na misitu, ambapo Afrika iliahidi kuchangia hekta milioni 100. Katika hizo, amesema Tanzania iliahidi kuchangia hekta milioni 5.2 mwaka 2018.

“Katika hili, kama nchi tunaboresha mifumo ya usimamizi wa rasilimali zetu, kufanya shughuli za kutunza ardhi ya misitu, kubadilisha na kurekebisha kanuni, sera na sheria zinazoratibu usimamizi wa matumizi ya rasilimali za misitu,” alisema.

Waziri wa Mazingira na Maendeleo Endelevu wa Madagascar, Max Fontaine amesema kuwa nchi wanachama wanahitaji kushirikiana katika utunzaji wa uoto wa asili na ardhi.

Ametolea mfano wa Madagascar ambapo asilimia 75 ya wakazi wake wanaishi maeneo ya vijiji na mikakati inaendelea kuhakikisha hawaharibu misitu na ardhi.

Kwa upande wake Sharon Ringo, balozi wa utalii Afrika Mashariki, amesema kila mwaka mamilioni ya hekta za misitu yanapotea. Amehimiza ushirikiano kati ya wananchi, Serikali, na sekta binafsi katika juhudi za kuiokoa misitu.

Related Posts