Mjadala wa bajeti 2024/2025: Sindano za moto zinazosubiri majibu

Dodoma. Wakati mjadala wa mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Sh49.35 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ukielekea mwishoni, hoja kadhaa ndio zimeongeza joto la kuilazimu Serikali kujipanga kikamilifu kuzijibu.

Hoja hizo zinaiweka Serikali kwenye kitanzi mbele ya watanzania kuona kama itasikiliza ushauri wa wabunge na kuziondoa kwa kuwa, zimelalamikiwa kuwa zinakwenda kuongeza makali ya maisha.

Saa chache baada ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kusoma Bajeti ya Serikali wachumi na wadau wa maendeleo walionyesha hofu kwa baadhi ya kodi mpya zilizopendekezwa kwa kuwa zinagusa moja kwa moja maisha ya watu wa kawaida.

Hata wabunge walipoanza kuchangia bajeti hiyo waligusa maeneo hayo hayo wakitaka Serikali kuondoa ama kupunguza kodi hizo kwa kuwa, zinakwenda kuongeza maumivu kwa wananchi.

Wabunge wengi wametaka kodi mpya ya Sh382 kwa kilo moja ya gesi ya magari, mchezo mchafu kwenye sukari ukomeshwe na ufike mwisho badala ya kila mwaka kuwa ngonjera zilezile za uhaba wa sukari na bei yake kupaa. Kikokotoo kwa miaka kadhaa sasa kimeendelea kuwa moto, madeni ya Serikali kwenye mifuko ya jamii.

Zingine ni ‘upigaji’ serikalini na watu kujificha kwenye kauli ya ‘mama anaupiga mwingi’, matumizi ya malipo kwa mfumo wa kidigitali, uhaba wa dola ya Marekani na ahadi ya Serikali kubana matumizi na madeni ya wakandarasi wa ndani na nje, ndio mambo yanayotikisa bungeni.

Mbunge Ester Bulaya alishikilia ‘bango’ hoja ya kikokotoo hadi kupewa jina na Halima Mdee la ‘Mama kikokotoo’.

Kwa upande wake, wabunge Joseph Kasheku ‘Musukuma’ (Geita Vijijini), Katani Ahmad (Tandahimba), Abubakar Asenga (Kilombero) na Elibariki Kingu (Singida Magharibi) walicharuka kuhusu sakata la sukari na kuunga mkono hoja ya Serikali ya kuipa jukumu Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuziba mianya ya uhujumu kunakowaumiza wananchi.

Serikali kwenye mapendekezo ya bajeti hiyo ya 2024/2025 kuongeza hadi asilimia 40 kutoka 33 kwa wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) na asilimia 33 hadi asilimia 35 kwa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), hoja imekuwa ni fomula inayotumika kwa mafao ya mkupuo.

Mdee ameilalamikia fomula ya mafao ya kustaafu kwa malipo ya mkupuo kwamba zamani ilikuwa inagawanywa kwa 540, lakini mpya ambayo ndiyo inapunja malipo ya mkupuo inagawanywa kwa 580.

Pia, wabunge walitaka nyongeza ya mishahara inayofanywa na Serikali ifanyike pia kwa wastaafu kwa kuongeza pensheni zao za kila mwezi kwani, tangu kustaafu kwao miaka mingi iliyopita wanapokea kiwango hicho hicho kwa miaka yote.

Hatua ya Serikali kuweka kodi katika gesi ya kwenye magari inatajwa kuwa maumivu mapya kwa wananchi.

Wabunge na wachumi kwa nyakati tofauti wameiita kodi hiyo kama bomu kwa kuwa inakwenda kinyume na hamasa ya watu kufunga mifumo ya gesi kwenye magari.

Charles Mwijage ameitaka Serikali kuondoa kodi hiyo na badala yake ifikirie kuweka ruzuku kwenye vifaa vinavyotumika kufunga mifumo ya gesi kwenye magari.

“Tumekosea na na naomba waziri unisikilize kwa nini unaweka ongezeko la pesa kwenye gesi, kwa nini gesi na watu wengi hawataki kuzungumza sisi gesi kwetu ni kinga. Ni usalama endapo kuna tatizo kwenye ugavi wa mafuta, sisi nchi tutabaki salama.

“Dawa ni kuwahimiza Watanzania watumie gesi nyingi tuwape kichocheo kusudi, moja tuwe salama kwa vyombo vya usafiri, pili itakapotokea tatizo hatutakuwa na tatizo, lakini mnatafuta pesa mbona mnaziacha zinapita,” alisema Mwijage.

Mdee yeye alisema petrol na dizeli bei zake Serikali haiwezi kudhibiti kwa kuwa uzalishaji wake unafanyika nje ya nchi.

Alisema matumizi ya gesi asilia kwenye magari kungesaidia kuondoa suala la mfumuko wa bei unaosababishwa na upandaji wa bei za mafuta duniani.

“Ongezeko la bei ya gesi gharama za usafiri na usafirishaji pia huongezeka, na hivyo kusababisha mfumuko wa bei kwa bidhaa na huduma nyingine. Mabadiliko haya yanaweza pia kuongeza gharama za bidhaa za kila siku, ambazo tayari zimekumbwa na hali ngumu ya kiuchumi,” alisema Mdee.

Sakata la bei ya sukari limezungumzwa na wabunge wengi huku wakisema kwa zaidi ya miaka 25 Watanzania wamekuwa watumwa wa bei ya sukari.

Wamesema kila aliyeshika nafasi ya Waziri wa Kilimo alikutana na tatizo la kuadimika sukari na bei kupanda kiholela na ameunga mkono hoja ya kuipa jukumu NRFA.

Kwa upande wake, Joseph Kasheku (Musukuma) yeye alisema: “Suala la sukari ni kubwa na limekua na kelele nyingi sana kila mwaka, nakumbuka mwaka 2019 wakati Waziri wa Kilimo akiwa Tizeba (Dk Charles Tizeba), na Waziri wa Biashara alikuwa Mwijage (Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage), walitoa sukari kwenye maghala kwa kutumia bunduki.

“Nishauri tunapoona kama suala hili linawakera wananchi ni vizuri tukabadilisha sheria ili haya masuala yakae vizuri, watu wakaacha kuwa kwenye taharuki.”

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby aliibuka na hoja kwamba wapo ‘wapigaji’ (wabadhirifu) wengi ambao wanasikika wakisifia kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi kumbe wanaiba fedha nyingi.

“Nchi imefikia mahali ambapo sasa hivi lazima tuseme ukweli. Wapigaji wamekuwa wengi. Wengine utawasikia wanasema Mama anaupiga mwingi, siyo kwamba (Mama) anaupiga mwingi wanamsifia kwenye moyo, anaupiga mwingi yeye (mpigaji) anaiba hela,” alisema Shabiby.

Alimtaka Dk Mwigulu kupenda watu wanaomwambia ukweli kama yeye na kwamba, alitaka kujikita katika barabara.

Alisema ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu alisema kuna barabara zilizochoka 71 ambazo muda wake umekwisha na ziko hoi.

“Ukichukua mfano wa Shinyanga, Mwanza, Lindi Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma ziko nyingi tu ukiangalia barabara ambazo mmepangia Wizara ya Ujenzi ni Sh1.7 trilioni, lakini madeni ni Sh1.2 trilioni. Hiyo ina maana wizara itabaki na Sh500 bilioni hiyo itafanya nini?,” alihoji.

Moja ya sababu za makali ya maisha kwa watanzania ni sakata la uhaba wa dola ya Marekani. Licha ya uimara wa uchumi wa Tanzania, lakini kuimarika kwa dola kumekuwa na athari kubwa na kusababisha mfumuko wa bei.

Hata hivyo, gesi asilia ambayo imekuwa ikionekana kama mkombozi dhidi ya kupaa kwa bei ya mafuta, nayo inapanda bei hivyo kuondoa ari ya watu kubadili mifumo.

Tanzania imekuwa ikitumia fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa nje ikiwemo mafuta, ambapo Serikali imepiga marufuku matumizi ya dola kwa huduma za ndani.

Hata hivyo, wabunge wameitaka Serikali kutazama upya matumizi ya gesia asilia inayozalishwa nchini kwamba, itapunguza matumizi ya dola katika kununua mafuta.

Pia, aliishauri Serikali kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa za ndani ili kupunguza utegemezi wa kuagiza nje jambo litakalosaidia kuokoa fedha za kigeni.

Wabunge wameililia Serikali kwamba wakandarasi wa ndani hawajalipwa madeni yao kwa kuda mrefu hali inayosababisha wafilisike kutokana na mikopo ya mitaji benki. Na kuhoji pengine ucheleweshaji unatokana na kutokuwepo riba kwa madeni yao.

Walitaka Serikali kuweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba wakandarasi wa ndani wanapata malipo yao kwa wakati ili kuendelea na miradi yao. Hii itasaidia kukuza uchumi wa ndani na kuhamasisha uwekezaji zaidi.

Related Posts