MAJALIWA: TUTAYAENZI MEMA YOTE YALIYOFANYWA NA NZUNDA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali na Watanzania wataendelea kumkumbuka na kuyaenzi mema yote yaliyoyafanywa na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Tixon Nzunda.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 21, 2024) alipokwenda kuhani msiba wa marehemu Nzunda, nyumbani kwa marehemu Goba, Dar es Salaam. Marehemu Nzunda alifariki Juni 18, mwaka huu kwa ajali ya gari.

“…Tunajukumu la la kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ailaze roho ya marehemu Nzunda pahala pema, pia tunajukumu la kuipa faraja familia yake.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema kuwa uwezo aliokuwa nao Marehemu Nzunda ulikuwa wa aina yake na ni pigo kutokana na kazi kubwa aliyokuwa akiifanya.

Amesema kuwa vijana wengi walijifunza kutoka kwake. “Sisi tunamengi ya kusema kama ushuhuda wa yale aliyoyafanya katika kipindi chote cha uongozi wake.”

Awali, mtoto wa marehemu, Victor Nzunda alisema marehemu baba yao aliwaasa waishi maisha ya kufanya ibada. “Baba yetu alikuwa mcha Mungu.”

Victor alisema baba yao alikuwa akiwaunganisha watu wenye mahitaji wakiwemo yatima na wazee pamoja kwenda hospitali kwa ajili ya kuwafariji wagonjwa.





Related Posts