MSHAMBULIAJI aliyemaliza mkataba na Yanga, Keneddy Musonda ameweka bayana sababu ziliyomfanya ashindwe kufanya vizuri ndani ya kikosi hicho, akidai ni presha kubwa iliyokuwa juu yake baada ya kuondoka kwa Fiston Mayele, kisha akatoa msimamo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi.
Musonda alibaki Yanga akiwa mshambuliaji tegemeo baada ya kuondoka kwa Mayele aliyetimkia Pyramids ya Misri akiwa mfalme wa upachikaji mabao akiifungia timu hiyo mabao 17 na kuibuka mfungaji bora ligi kuu sambamba na Saido Ntibazonkiza aliyekuwa Simba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Musonda alisema changamoto kubwa iliyomwangusha na kushindwa kuwa bora msimu ulioisha ni kushindwa kuhimili presha ya kujivika kinyago cha kuwa mchezaji tegemeo katika safu ya ushambuliaji na kujikuta akiishi kwa presha kubwa.
“Sikuwa na msimu bora, nilihitaji zaidi mwanasaikolojia kuliko kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, nilijitahidi kupambana kwa uwezo wangu lakini mambo yalikuwa magumu, kwangu nakiri kushindwa kufikia malengo,” alisema Mzambia huyo aliyemaliza msimu na mabao manne ya Ligi Kuu na moja la michuano ya Kombe la Shirikisho.
“Timu ilikuwa na wachezaji wengi wazuri na nilikuwa nazungukwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kunitengenezea nafasi lakini sikuweza kuwa bora hilo naamini ni kutokana na presha kubwa niliyokuwanayo kutoka kwa mashabiki ambao walitamani kuona mimi nakuwa Mayele kitu ambacho hakikuwa rahisi kwangu,” aliongeza Musonda.
Nyota huyo alisema ubora wa Yanga licha ya kushindwa kupachika mabao mengi kama ilivyotarajiwa ulimfichia mambo mengi na amefurahi kuona timu hiyo ilifanikiwa kutetea taji bila ya uwepo wa Mayele ambaye tayari alijitengenezea rekodi nzuri.
“Unajua kuondoka kwa Mayele nami kubaki kila shabiki wa Yanga aliamini ndio nitaongoza safu ya ushambuliaji mambo yakawa tofauti kiungo mshambuliaji ndiye aliyeokoa jahazi na kunifichia madhaifu yangu, kubwa ninaloshukuru ni timu kutwaa ubingwa,” alisema Musonda na kuongeza;
“Nafurahi kucheza na wachezaji ambao hawakutaka nikubali kuwa jukumu langu ni kufunga tu, walikuwa pamoja na mimi na kunipa sapoti hadi hapo tulipofikia lengo la kumaliza msimu kwa kutetea taji na kutoa mfungaji bora ndani ya timu ambayo wengi hawakutarajia baada ya kuachana na staa wao ‘Mayele’,” alisema.
Akizungumzia mkataba na Yanga alisema amemaliza na hakuna mazungumo mapya hadi sasa na kuhusu kucheza tena Tanzania lolote linaweza kutokea bila ya kutaja ni timu gani anaweza kucheza msimu ujao.
“Nimemaliza mkataba na Yanga, nilisajiliwa kwa miaka miwili msimu uliopita na huu ulioisha hivi karibuni, hivyo kwa sasa ni mchezaji huru na kuhusu kucheza Tanzania lolote linaweza kutokea japo hadi sasa sijajua ni timu gani, lakini muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi,” alisema Musonda.
Mshambuliaji huyo msimu ulioisha amepachika kambani mabao manne akifunga dhidi ya JKT 5-0, Simba 5-0, Mtibwa 4-0, Mtibwa 3-1.
Dakika alizocheza KMC (64), JKT (78), Namungo (90), Geita Gold (17), Singida Big Stars (18), Simba (72), Coastal Union (59), Mtbwa (30), Tabora United (64), Kagera Sugar (34), Dodoma Jiji (61), Mashujaa (22) KMC (30), JKT (80), Ihefu (60), Geita Gold (90), Simba (18), Coastal (90), Mtibwa (90).