Dar es Salaam. Unaweza kusema mambo bado baada ya Muswada wa Sheria ya Fedha kwa mwaka 2024, kuwasilishwa bungeni ukiwa haujabeba masuala ambayo wengi walitamani yabadilishwe katika mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025.
Zikiwa zimebakia siku chini ya 10 kabla ya mwaka mpya wa fedha kuanza Julai Mosi, matumaini ya wengi sasa yamebakia kwa wabunge ambao ndio wana jukumu la kuipitisha bajeti na muswada huo ili kuufanya kuwa sheria.
Muswada uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni, unapendekeza mapato yatokanayo na tofauti ya kushuka kwa bei za mafuta, yawekwe kwenye mfuko wa dharura wa kugharimia matengenezo ya dharura ya miundombinu ya barabara inayoharibika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia usajili wa magari ya umeme gharama yake imependekezwa kuanzia Sh95,000 hadi Sh250,000 kulingana na aina na ukubwa wake.
Mengine ni marekebisho kwenye Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ambayo kifungu cha 25(3) kinapendekezwa kurekebishwa, ili kuainisha kiwango cha ushuru wa bidhaa ambacho kitapelekwa katika Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.
“Inapendekezwa kiasi cha asilimia mbili kinachotokana na ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji laini, vileo na vipodozi kiwekwe katika mfuko huo,” alisema Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba katika maelezo ya muswada huo.
Muswada unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Sukari, ambapo kifungu kipya cha 14A kinapendekezwa kuongezwa kwa lengo la kuuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuagiza sukari, kuhifadhi na kusambaza kwa matumizi ya ndani ya nchi wakati wa upungufu wa sukari.
“Lengo la hatua hii ni kuwezesha upatikanaji wa sukari nchini na kuondoa uhodhi kwa baadhi ya wenye viwanda bila kuathiri dhamira ya Serikali ya kulinda viwanda vya ndani,” alieleza Dk Mwigulu.
Pia muswada unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura ya 220, ambapo kifungu cha 3 kinarekebishwa kwa kuiandika upya tafsiri ya msamiati “nishati” ili kujumuisha gesi asilia katika tafsiri hiyo.
Vifungu vya 4, 4A na jedwali la pili vinarekebishwa ili kutoza ushuru wa Sh382 kwa kila kilo ya gesi asilia inayotumika kwenye magari, huku mapato yatakayotokana na ushuru huo yakipelekwa katika Mfuko wa Barabara.
Dk Mwigulu anasema lengo la marekebisho hayo ni kuongeza mapato yatakayotumika katika kufanya matengenezo ya barabara na kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta, tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Kwa mujibu wa Bunge, Kamati yake ya Kudumu ya Bajeti itasikiliza maoni ya wadau kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia Juni 23 hadi Juni 25, mwaka 2024.
Hata hivyo, hoja ya kuipa NFRA jukumu la kuagiza sukari na utozaji wa Sh382 katika gesi inayotumika kwenye magari, zimekuwa na mjadala mpana katika bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25.
Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Mwinuka Lutengano, alisema bajeti inayopendekezwa na Serikali ina mambo mazuri na mengine ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi zaidi ili kuleta maendeleo.
Dk Lutengano alisema kuna maeneo yenye fursa kubwa katika ukusanyaji lakini yanachangia kiduchu, hayo yakifanyiwa kazi bajeti itaweza kuleta manufaa ya kiuchumi yanayotamaniwa.
“Kwenye mapato ya jumla Serikali za mitaa zinachangia kidogo wakati zina uwezo wa kubuni miradi na kuchangia zaidi hata eneo la mikopo nafuu na misaada likitumiwa vizuri linaweza kuleta mchango mkubwa kuliko mikopo ya kibiashara,” alisema na kuongeza kuwa msisitizo unapaswa kuwekwa katika suala hilo.
Alisema katika utekelezaji wa baadhi ya miradi, Serikali inapaswa kuweka kipaumbele zaidi kwenye ubia wa sekta ya umma na binafsi ili pesa zinazofanya miradi hiyo sasa zifanye ile ambayo haina masilahi kibiashara.
Kuhusu udhibiti wa sukari, suala ambalo limeibua mjadala baada ya mapendekezo yaliyotolewa katika bajeti, Dk Lutengano alisema ni mpango mzuri isipokuwa ni muhimu kuhakikisha NFRA inakuwa na uwezo iliopatiwa.
“Sasa hivi NFRA ina jukumu kubwa la kununua mahindi lakini bado haifanyi kwa kiwango kinachotamaniwa, hivyo pamoja na uzoefu wake na nia yake njema ni vyema Serikali ikaongeza uwezo wake ili kutimiza jukumu hilo vizuri,” alisema Dk Lutengano.
Mhadhiri wa masuala ya fedha wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai, alisema miongoni mwa mabadiliko ya sheria yaliyofanywa katika muswada huo ni ya muhimu katika kuhakikisha bajeti pendekezwa inatekelezeka.
“Nimeangalia zinazohusiana na benki na taasisi ndogo za fedha nilichoona ni kuwa wanataka kutoza kodi siyo kwa riba pekee bali kwa mapato mengine, nafikiri siyo kitu kibaya kwa sababu inatakiwa kweli yatozwe kodi,” alisema Dk Swai.
Alichosema Profesa Wangwe
Naye mchambuzi na msomi bobezi wa uchumi, Profesa Samuel Wangwe anazungumzia maeneo matatu ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi kabla ya bajeti kupitishwa akitaja suala la udhibiti wa sukari, CNG na ongezeko la mapato.
Profesa Wangwe alisema kwa suala la sukari badala ya kujikita katika udhibiti wa usambazaji, bajeti ingeweka nguvu zaidi katika kuweka mazingira rafiki ya kuongeza uzalishaji wa viwanda vya ndani.
“Kudhibiti usambazaji siyo suluhu ya kudumu bajeti inapaswa kujikita zaidi katika kusaidia viwanda kupanuka ili sukari ipatikane kwa wingi siyo mjadala wa uingizaji,” alisema.
Kuhusu tozo ya Sh382 katika gesi asilia, alisema hicho siyo kitu cha kuanza kutozwa kodi sasa kwa kuwa kilikuwa kinaleta unafuu mkubwa kwa watu na kupunguza utegemezi wa nishati muhimu kutoka nje ya nchi.
“Bajeti ilipaswa kuja na majibu ya kwa nini vituo vya mafuta vinaongezeka kila siku lakini vya gesi haviongezeki? Iweke mkakati wa kuviongeza, watumiaji wakishakuwa wengi ni sawa kuwatoza kuliko sasa, kodi yenyewe itakayokusanywa ni ndogo na itapunguza mwamko wa wengi kuhamia huko,” alisema Profesa Wangwe.
Alisema ili kupunguza changamoto za kibajeti na kikodi, ni vyema sasa wabunge wakapewa jukumu la kuchechemua uchumi katika maeneo wanayotoka ili hoja za kitaifa wanazozitoa zianzie kwenye maeneo yao.
“Tunapaswa kupunguza kutegemea Dar es Salaam tu katika bajeti, tuweke mazingira ya kukusanya nchi nzima, wabunge wafanye kazi ya kupunguza umasikini katika maeneo yao kwa kuvutia uwekezaji na shughuli za kiuchumi,” alisema Profesa Wangwe.