LIGI Kuu ya Wanawake (WPL) imemalizika mapema wiki hii kwa Simba Queens kubeba taji la nne tangu kuasisiwa kwa michuano hiyo mwaka 2016, kuashiria kufungwa kwa msimu wa 2023-2024 na klabu kwenda mapumziko kujiandaa na msimu ujao wa 2024-2025.
Ligi hiyo imeisha ikiacha gumzo kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo kwa klabu 10 shiriki na Simba ilipindua meza mbele ya JKT Queens waliokuwa wanaoongoza kwa muda mrefu mwanzoni mwa msimu kabla ya kupigwa rungu na TFF kwa kupokwa ponti tano zilizoiporomosha.
Ushindani wa ligi hiyo ulichagizwa na mambo mengi ikiwemo ubora wa baadhi ya wachezaji na huenda wakagonganisha timu zitakazohitaji saini zao na tayari dirisha la usajili kwa ajili ya msimu ujao limeshafunguliwa tangu Juni 15 na litafungwa Agosti 15.
Mwanaspoti limekuchambulia baadhi ya wachezaji wa watakaokuwa lulu sokoni kutokana na viwango walivyoonyesha msimu uliomalizika.
1. Precious Christopher (Yanga Princess)
Miongoni mwa wachezaji gumzo kutokana na ubora walionyesha msimu huu licha ya Yanga kutokufanya vizuri. Amekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi hicho eneo la kiungo.
Alijiunga na Yanga Septemba 10, 2022 akitokea Rivers United ya Nigeria kwa mkataba wa miaka miwili na unatamatika msimu huu na anaweza kucheza timu yoyote kulingana na kiwango alichoonyesha.
Mnigeria huyo amefunga mabao matatu WPL kwenye mechi 14 na anamudu kucheza nafasi mbalimbali ikiwemo straika, kiungo mshambuliaji na mlinzi wa kushoto.
2. Amina Bilal (JKT Queens)
Alijiunga na JKT msimu uliopita akitokea Yanga akichukua kandarasi ya mwaka mmoja unaoisha mwishoni mwa msimu huu.
Kutokana na kiwango alichoonyesha msimu huu akiwa na JKT, anahusishwa tena na kujiunga Yanga ikihitaji saini yake wakimtazama kuja kuchukua nafasi ya Mzungu Kaeda Wilson aliyerudi Marekani kwa ajili ya masomo.
3. Anitha Adongo (Alliance Girls)
Licha ya Alliance kusuasua kwenye Ligi Kuu, lakini nahodha wa timu hiyo, Anitha amekuwa na kiwango bora kwenye eneo la ulinzi.
Mchezaji huyo raia wa Kenya anawindwa na timu nne, Simba Queens, Yanga, Ceasiaa Queens na Fountain Gate zikihitaji saini ya beki huyo ambaye ana uwezo wa kukaba.
4. Noela Luhala (Yanga Princess)
Ukitaja majina ya wachezaji wanaofanya vizuri kwa sasa eneo la ulinzi huwezi acha kumtaja Noela ambaye amekuwa silaha kubwa kwa wananchi hao.
Ni miongoni mwa wachezaji wanaomaliza mkataba na Yanga msimu huu na uwezo wake wa kukaba umewavutia Simba wakihitaji saini yake akihusishwa pia na timu kutoka Uarabuni.
5. Winifrida Gerald (JKT Queens)
Winga huyo wa timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20 ni msimu wake wa mwisho JKT baada ya kuitumikia kwa mwaka mmoja akitokea Fountain Gate Princess.
Hadi sasa amefunga mabao manane akiwa kwenye tatu bora za vinara wa mabao WPL licha ya kutopata nafasi kubwa ya kucheza kutokana na ushindani aliokutana nao kwenye eneo la ushambuliaji.
Kutokana na uwezo alioonyesha kwenye kikosi hicho inawezekana akasajiliwa na timu kubwa za Simba na Yanga ambazo kwa umri wake na kiwango chake anaweza kuwasaidia.
6. Hasnath Ubamba (Fountain Gate Princess)
Licha ya Fountain msimu huu kuonekana imepunguza ushindani lakini uwezo wa straika huyo mwenye mabao matano Ligi Kuu umekuwa msaada kwenye kikosi hicho.
Ni fundi kweli kweli wa kupachika mabao na uwezo wake unaweza kumfanya asiendelee kuwepo kwenye kikosi chake kwani amekuwa akihusishwa na JKT, Yanga na Simba.
7. Aisha Mnunka (Simba Queens)
Huu unaweza kuwa msimu bora kwa Aisha baada ya kufunga mabao 20 na kuibuka mfungaji bora wa ligi hiyo.
Alionyesha kiwango bora na sokoni atakuwa lulu kwani kwenye suala la upachikaji mabao hashikiki.
8. Sara Joel (Fountain Gate Princess)
Msimu uliopita alichukua tuzo ya beki bora wa kulia na ni mchezaji muhimu kwenye kikosi cha timu ya taifa ya wasichana U-18.
Msimu huu hakucheza sana kwenye ligi kutokana na kusumbuliwa na majeraha na ni miongoni mwa wachezaji wanaomaliza mkataba msimu huu na Fountain.
Hadi sasa tayari Simba, Yanga na JKT zimetuma ofa kwa beki huyo kutaka saini yake kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali.
Mbali na vigogo wa WPL, pia amezivutia baadhi ya klabu nchini Uganda ikiwemo Kampala Queens ambayo tayari imetuma mwakilishi kuja Tanzania kumalizana naye.