Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), imetangaza ruti mpya za daladala kutoka Kigamboni kwenda katikati ya jiji ikihusisha Kigamboni – Stesheni, Kigamboni – Mnazi Mmoja na Kigamboni Muhimbili.
Tangazo la ruti hizo limetolewa jana Juni 21, 2024 kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram wa mamlaka hiyo.
Daladala zinazotakiwa kuingia barabarani katika ruti hizo ni 25 kwa kila njia, huku vigezo vikiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria kuanzia 20.
Hatua hiyo inakuja zikiwa zimepita wiki mbili tangu Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa), kutangaza kusitisha huduma za kivuko cha MV Kigamboni kwa ajili ya kukifanyia matengenezo.
Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Latra, Salum Pazi, ameliiambia Mwananchi kuwa uamuzi huo hauna uhusiano na kuharibika kwa vivuko isipokuwa kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya wananchi la usafiri katika njia hizo.
“Kazi yetu ni kuwafanya wananchi kupata huduma ya usafiri kwa wepesi na katika njia hizo hakukuwa na daladala jambo lililofanya bajaji kutumia kama fursa wakati wakijua wao ni usafiri wa kukodi na sio kutoa huduma kama wanavyofanya sasa
“Hivyo mbali ya kuwasogezea huduma wananchi lakini pia tunataka kuondoa tabia ya bajaji kujigeuza daladala kusafirisha watu kama ndio usafiri wa umma huku ikiwatoza bei kubwa,” amesema Pazi.
Katika tangazo lililitolewa Juni 6, 2024 na Tamesa ilitaja sababu za kusitisha huduma za kivuko cha MV Kigamboni kuanzia Juni 7 kwa na kueleza kinakwenda kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Kutokana na hatua hiyo, wakala huo ulitaarifu kuwa huduma za uvushaji abiria katika eneo la Magogoni-Kivukoni, zitaendelea kutolewa na Kivuko cha MV Kazi na Sea Tax.
Aidha, kwa wenye magari walitakiwa kutumia njia mbadala kupitia Daraja la Mwalimu Nyerere ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na MV Kigamboni kutokuwepo.
Hata hivyo tangu kivuko hicho kisimame kikitanguliwa na kile cha MV Magogoni kilichoenda matengenezo tangu mwaka jama, hali ya usafiri katika eneo hilo sio nzuri kwani wananchi wanalazimika kutumia mitumbwi kuvuka huku kivuko kimoja tu cha Mv Kazi ndicho kinachotoa huduma kwa sasa.
Baadhi ya wananchi wakizungumzia hatua hiyo akiwemo Zuhura Jamal, mkazi wa Kigamboni, wamesema daladala zitawasaidia zaidi wanaokaa maeneo ambayo wanalazimika kupita darajani na kuomba tatizo la vivuko kufanyiwa kazi haraka.
Edwin Lubiga, mkazi wa Nunge amesema hiyo kwao ni habari njema kwa kuwa awali ili uweze kufika mjini ilipaswa uwe na sio chini ya Sh3,000 huku usafiri mkubwa ukiwa ni bodaboda.
“Kwa hali zetu za maisha wananchi wa chini kila siku kuwa na hiyo hela ni shida,kwani kuna kipindi unapanda ya Machinga Complex unashuka gerezani na kutembea kwa miguu hadi mjini, hivyo niipongeze Serikali kwa kuliona hili,” amesema Edwin.