ALIONDOKA uwanjani na kitambaa katika bega kama nahodha, tabasamu usoni. Sura chini. Mfupi kama alivyo, shujaa kama alivyo, N’Golo Kante alinikumbusha mbali katika pambano la majuzi kati ya Ufaransa dhidi ya Austria kule Ujeumani. Kwamba N’Golo ni yule yule tu.
Baada ya pambano aliingia katika vyumba vya kubadilishia nguo na wachezaji wenzake wakaanza kumshangilia. Mchezaji Bora wa mechi. Ndio, Mchezaji Bora wa mechi katika pambano la kwanza la Euro 2014. Alitukumbusha namna ambavyo dunia haimdai. Alitukumbusha N’Golo ni yule yule tu.
Wenzake wote wanacheza Ulaya katika klabu mbalimbali ambazo nyingi kati ya hizo ni kubwa. Wana majina makubwa. Kina Kylian Mbappe aliyeondoka uwanjani akiwa amevunjika pua. Kina Antonio Griezmann, Olivier Giroud na wengine lukuki.
Kitu ambacho kingedhaniwa na ambacho kina asilimia ya ukweli ni ukiondoka Ulaya katika nyakati hizi ambazo mpira umeongezeka ushindani, inakuwa ngumu kuitwa katika timu ya taifa kwa sababu ushindani wa Ulaya ni tofauti na Saudi Arabia.
Hapo hapo hata kama mchezaji akiitwa inakuwa ngumu kuwa katika makali zaidi kwa sababu anakumbana na rundo kubwa la wachezaji, kuanzia wenzake hadi wale wanaocheza Ulaya, ambao wanatoka katika soka la kishindani zaidi kuliko yote.
Zaidi ya haya ni wachezaji wengi ambao wamekwenda Saudi Arabia inaonekana umri na ushindani wa kucheza Ulaya umekuwa kikwazo kwao. Lakini hapo hapo N’Golo akaingia katikati ya hisia zetu na kuondoka uwanjani akiwa mchezaji bora wa mechi.
Kumbe N’Golo ni yule yule tu. Inasemwa kwa utani kule Ulaya ‘Asilimia 75 ya dunia inatawaliwa na maji, asilimia 25 iliyobakia inamilikiwa na N’Golo Kante’. Hiki ndicho ambacho kwa kiasi kikubwa ametuonyesha.
N’Golo ni yule yule tu. Hajabadlika. Ametuonyesha hili. Kwamba anaweza kurudi Ulaya wakati wowote ule na kuendelea kufanya alichokiacha. Ni basi tu aliamua kwenda zake kuchukua noti za Waarabu huku tukiwa hatuna chochote tunamchomdai.
Kuna wachezaji ambao wamekwenda Saudi Arabia huku tukiwa tunawadai. N’Golo sio mmoja wao na anaweza kutusuta kwa sababu mbalimbali. Kwanza kabisa ameenda zake Saudi Arabia huku akiwa ni mchezaji anayependwa zaidi na mashabiki wa timu zote na sio tu ile aliyoondokea, Chelsea.
Ameondoka akiwa hana kadi nyekundu, huku akiwa na kadi za njano za kijinga. Ameondoka akiwa hajakunjana mashati na wachezaji wa timu pinzani wala wa timu yake. Ameondoka akiwa ameinamisha kichwa chini huku shingo yake ikiwa imejaa medali.
Katika hili la medali N’Golo ameondoka England akiwa na mataji mawili ya Ligi Kuu. Kama unadhani taji lake la pili akiwa na Chelsea liliambatana na ukweli alikuwa anacheza katika klabu kubwa sambamba na wachezaji wakubwa basi kumbuka taji lake la kwanza akiwa na Leicester City. Alichukua msimu ule akiwa na wachezaji wa kawaida, huku yeye akiwa mhimili mkubwa zaidi.
Nini zaidi tumdai N’Golo? Ligi ya Mabingwa. Alitwaa pia na Chelsea. Kuna taji kubwa zaidi ya Kombe la Dunia? Alitwaa na Ufaransa mwaka 2018. Wachezaji wenzake walilazimika kumpelekea taji ili alinyanyue kwa sababu wakati wenzake wakishangilia yeye alikuwa kando akiwatazama kwa aibu.
Ana mataji mengine lukuki. Ana tuzo binafsi pia. Huyu ndiye N’Golo ambaye alirudi wiki hii na kuwa mchezaji bora wa pambano la Ufaransa dhidi ya Austria.
Baada ya kila kitu alichofanya Ulaya N’Golo alistahili tuzo nyingine kubwa. Tuzo ya pensheni. Washauri wake pamoja na kampuni inayomsimamia wakaona bora aende zake Saudi Arabia kuchukua noti za Waarabu. Halikuwa jambo baya. Tunamdai nini N’Golo?
Kwa Chelsea wenyewe, N’Golo aliondoka katika kipindi cha mpito. Kipindi ambacho Roman Abramovich alikuwa ameingia matatizoni na serikali ya Uingereza kiasi cha kunyimwa visa ya kuingia nchini humo. N’Golo aliondoka katika kipindi ambacho Chelsea ililazimika kuundwa upya.
Wachezaji wakaondoka, tajiri akaondoka, chawa wa tajiri wakaondoka. Yeye angesubiri nini zaidi? Ni mashabiki tu ndio huwa wanabakia klabuni katika nyakati kama hizi. Sijawahi kusikia popote pale mashabiki wa Chelsea wakilaumu kuondoka kwa N’Golo hasa ukizingatia mkataba wake ulikuwa umeisha.
Sisi wengine ambao sio mashabiki wa Chelsea hatukuwa na tatizo lolote la N’Golo kuondoka kwa sababu halikuwa suala letu. Sana sana tulikuwa tunashangilia namna ambavyo mchezaji kama yeye alikuwa anaondoka huku akiitia udhaifu Chelsea. Maisha bila ya unafiki hayaendi. Kwani Chelsea imefanya kitu gani cha ajabu baada ya N’Golo kuondoka?
Anastahili noti za Waarabu. Mwache aendelee kuzipata. Amekuja Euro kutukumbusha tu kama angeendelea kucheza Ulaya basi muziki wake ungeendelea kuwa ule ule tu. Pia anamkumbusha kocha wake wa Ufaransa, Didier Deschamps namba yake haijapata mbadala.
Pamoja na kila kitu. Pamoja na kipaji chake. Baada ya michuano hii N’Golo anaweza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa. Lakini anatukumbusha kuna wachezaji wachache ambao hawakuchezea timu yako lakini hauwezi kuwachukia.
Iwe klabu au timu ya taifa lakini hauwezi kuwachukia. N’Golo Kante ni mmoja wapo. Mpole, mchapakazi, hana shida na mtu. Hauwezi kumchukia. Ukikutana naye utampa mkono na kumsalimia lugha ya kwao Kifaransa. Utampa mkono tu na kumwambia ‘Coma Sava’. Hauwezi kumpita hivi hivi bila ya kuomba kupiga naye picha. Unaweza kuwa mrefu zaidi yake lakini yeye ni shujaa.