Musoma. Ustaadh wa msikiti wa Aljazeera uliopo katika Mtaa wa Nyabisare, manispaa ya Musoma mkoani Mara ameingia matatani kwa tuhuma za kumfanyia ukatili na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili mtoto wake wa kumzaa.
Ustaadh huyo, Issa Mgema (30) anadaiwa kumfanyia ukatili kwa kumpiga na kumchapa na waya wa umeme sehemu mbalimbali za mwili mtoto huyo wa kiume, mwenye umri wa miaka sita kwa nyakati tofauti nyumbani kwake.
Alipotafutwa kuulizwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi.
Amesema taarifa za awali zinadai baba huyo amekuwa akimuadhibu mtoto huyo kutokana na hasira kufuatia tabia ya mtoto huyo ya kumuibia fedha mara kwa mara, na kwamba baada ya kumwadhibu mtuhumiwa alikuwa na tabia ya kumfungia mtoto huyo ndani.
Baadhi ya majirani ambao hawakutaka majina yao yaandikwe, wamedai ustaadh huyo amekuwa na tabia ya kumchapa mara kwa mara mtoto huyo, jambo ambalo wamedai linakiuka haki za msingi za mtoto.
“Tunaomba mtusaidie, vitendo anavyovifanya baba huyu kwa mtoto havikubaliki na tena havivumiliki, amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara. Mimi kama mzazi naumia kwa kweli,” amesema jirani mmoja.
“Huyu mtu aliletwa hapa na uongozi wa msikiti kama msimamizi na alikuwa na mke wake ambaye ndiye mama wa mtoto huyu, lakini waliachana kisha akaoa mwanamke mwingine, naye wakaachana na sasa ana mwanamke mwingine lakini tabia yake sio nzuri. Amekuwa akimuadhibu mtoto huyu mara kwa mara,” amesema jirani mwingine.
Mwananchi lilifika katika makazi ya ustaadh huyo leo Ijumaa Juni 21, 2024 na kumkuta mtoto huyo akiwa na majeraha na alama za viboko maeneo ya mgongoni, mashavuni, miguuni na tumboni.
Alama za mgongoni na mashavuni zilikuwa bado hazijapona vizuri, hali inayoonyesha kuwa majeraha hayo ameyapata siku za hivi karibuni.
Mtoto huyo anayesoma darasa la kwanza anadaiwa kuwa muoga kutokana na vipigo ambavyo amekuwa akivipata mara kwa mara, hali ambayo imemfanya asipende kukaa karibu na watu.
Akizungumzia madai hayo, Ustaadh Issa amekiri kumchapa mtoto huyo ingawa amekanusha madai ya kuwa amekuwa akimchapa mara kwa mara.
“Ni kweli nilimuadhibu lakini ni mara mbili tu na mara ya mwisho ilikuwa ni wiki moja iliyopita na wala sikuwa na lengo baya, nilitaka tu kumwadabisha mtoto baada ya kuona ana tabia mbaya.
“Unajua wanasema usitoe hukumu ukiwa na hasira na hiki ndicho kilichonikuta kwani nilijikuta namchapa hadi kupitiliza, lakini baada ya kuona amepata majeraha nilimtibu kwa kumpa dawa hapa hapa nyumbani,” amesema ustaadhi huyo.
Akieleza makosa ya mtoto huyo yaliyosababisha ampe adhabu, Ustaadh Issa amesema mwanaye amekuwa na tabia mbaya ikiwa ni pamoja na kuongozana na watoto ambao wanadaiwa kuwa wadokozi mtaani hapo.
“Imefika hatua hata darasani alikuwa haingii na niliitwa shuleni nikaongea naye lakini naona hakunielewa, akawa anaendelea na tabia hiyo, hapo ndipo nilipomchapa mara ya kwanza,” amesema Ustaadh Issa, baba wa watoto wawili.
“Mara ya pili nilimchapa baada ya kumuita akakimbilia chooni na hii ni mara ya pili kwani mara ya kwanza pia nilimuita akakimbilia chooni, nilipomtafuta nilimkuta amejifungia humo, kwa hiyo nikaona hii inataka kuwa tabia yake, ndipo nilipochukua fimbo na kuanza kumchapa,” amesema
Mama mlezi wa mtoto huyo Husna Issa (20), amesema mume wake alimchapa mtoto hadi kumjeruhi kutokana na hasira alizokuwa nazo na wala sio kitu kingine.
“Hii ni bahati mbaya alishikwa tu na hasira kwa sababu huyu mtoto amekuwa ni mkorofi, kila akielezwa jambo hasikii na badala yake anafanya yake anayozuiwa kufanya, mara hafiki shuleni, mara ajifungie chooni, kwa hiyo baba yake alitaka kumuadhibu, sema hasira zikazidi,” amesema.
Hata hivyo, mtoto huyo ameiambia Mwananchi Dijital kuwa sio mweli kuwa baba yake amekuwa akimchapa kwa kutumia fimbo, bali amekuwa akimchapa kwa kutumia waya wa umeme.
“Huo waya huwa anautunza kwenye meza na kila akitaka kunichapa anafunga mlango, mimi nataka kwenda kwa mama yangu, anaishi Ukerewe, sitaki kukaa hapa,” ameeleza mtoto huyo na kuongeza:
“Mara nyingi baba ndio huwa ananichapa na nikiumia kama hivi huwa ananikanda kwa kutumia shati lake ambalo huwa analiloweka kwenye maji ya moto na sio kweli kwamba ananipa dawa, ila mama yeye aliwahi kunichapa mara moja, baba ndio ananichapa mara kwa mara,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bweri, Rhoda Laurian amesema taarifa za mtoto huyo alizipata kutoka kwa wananchi wake, hivyo akalazimika kufika nyumbani kwa mtuhumiwa kwa ajili ya hatua zaidi.
“Ni kweli tukio lipo na mhusika mwenyewe amekiri na mtoto mwenyewe tumemkuta na majeraha yake, tayari nimetoa taarifa polisi ambao wameahidi kufika hapa muda si mrefu,” amesema Rhoda.
Mtendaji huyo ametoa wito kwa jamii kutokufumbia macho vitendo vya ukatili kwa watoto, kwani vina madhara makubwa katika ustawi wa jamii.
“Jamii isifumbie macho vitendo hivi, taarifa zitolewe ili wahusika wawe wanakamatwa kwani vitendo hivi vinasababisha kuwa na jamii iliyojaa ukatili baada ya watoto kuwa sugu kutokana na kufanyiwa vitendo vya ukatili kwa muda mrefu,” amesema.