Askofu Wolfang Rais mpya TEC, Padri Kitima aula tena

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetambulisha safu mpya za viongozi watakaoongoza baraza hilo kwa miaka mitatu hadi 2027 huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa baraza hilo, Padri Dk. Charles Kitima akirejeshwa tena kuendelea kutumikia nafasi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Baraza hilo limemtambulisha Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa OFM Cap ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi kuwa Rais mpya wa TEC. Askofu Wolfang amechukua nafasi ya Askofu Mkuu Gervais Nyaisonga ambaye amemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TEC katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, viongozi hao wametambulishwa leo Jumamosi muda mfupi baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya kuwatambulisha rasmi kama viongozi wapya wa Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Adhimisho limefanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili yalipo Makao Makuu ya TEC-Kurasini Dar es salaam.

Waliochaguliwa kwa ngazi za Askofu Wolfgang pamoja na Padri Kitima, wengine waliochaguliwa ni Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa (Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda) kuwa Makamu wa Rais TEC na Padri Chesco Msaga kuwa Naibu Katibu Mkuu TEC.

Padri Dk. Charles Kitima

Askofu Wolfgang Pisa ni nani?

Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alizaliwa tarehe 6 Julai 1965 huko Karatu, Jimbo Katoliki la Mbulu.

Baada ya masomo na malezi ya kitawa Lusaka, Zambia na Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro aliweka nadhiri za daima tarehe 15 Agosti 1998 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 1 Septemba 1999.

Tarehe 9 Aprili mwaka 2022 Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francisco, alimteua, Padre Wolfgang Pisa, kuwa Askofu wa Jimbo la Lindi. Kabla ya kuteuliwa kwake kuwa Askofu alikuwa Paroko-usu Parokia ya Kwangulelo Jimbo kuu la Arusha na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Tawi la Arusha.

Padri Chesco Msaga

Historia yake inaendelea kuonesha kuwa mwaka 2000 Rais huyo mpya wa TEC alitumwa na Shirika kujiendeleza zaidi katika masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hapo akajipatia Shahada ya Uzamili. Akateuliwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Maua kati ya mwaka 2005-2008.

Baadaye alijiendeleza zaidi katika masomo ya maadili Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Marekani, Catholic University of Amerika huko Washington, DC kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011. Akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wakapuchini Kanda ya Tanzania na kuwaongoza tangu mwaka 2011 hadi mwaka 2017.

Baadaye kati ya mwaka 20017-2019 akarejea tena darasani huko Catholic University of America huko Washington, DC na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Maadili. Amewahi kufanya shughuli zake za kichungaji Parokiani Kibaigwa, Jimbo kuu la Dodoma kati ya mwaka 2019-2020.

Tangu wakati huo, hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alikuwa ni Paroko usu wa Parokia Kwangulelo Jimbo kuu la Arusha na Jalimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, Tawi la Arusha.

Related Posts