Na Janeth Raphael- MichuziTv – Bungeni Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini Mhe. Jumanne Kishimba ameiomba serikali kuimarisha miundo mbinu ya barabara katika jimbo lake Kahama Mjini Mkoani Shinyanga ambayo imeharibika kwa kiasi kikubwa ili kuchochea wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi na kufanya biashara katika mazingira rafiki.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia hoja katika hotuba ya baejti ya kuu ya serikali.
Ameongeza kusema Jimbo la Kahama Mjini ndilo linaloongoza Tanzania katika uchangiaji wa mapato ya Serikali kwa njia ya mtandao na hivyo kufanya jimbo hilo kupata zawadi ya ushindi.
“Ninaomba Serikali kufikiria namna nzuri ya kurekebisha barabara zilizoharibika kwa Kuimarisha miundo mbinu,” alisema Kishimba.
Akizungumzia utoaji wa risti amesema sheria ya kuadhibu mtu kulipa shilingi milioni 15 au kwenda Gerezani au vyote viwili kwa pamoja bado hailengi kutatua tatizo kwa sababu anayekaa kwenye biashara ni mfanyakazi na si mfanyabiashara.
Amefafanua kama sheria inalenga kumfunga Mfanyabiashara kwa kosa la kutotoa risti ambalo limefanywa na mfanyakazi wake, kuna uwezekano mkubwa wa wanyabiashara wengi kukumbwa na adhabu.
Sheria inapaswa kuangalia vizuri upande wa mnunuzi ambaye anapaswa kudai risti, badala ya kuangalia upande wa wafanyabiashara lazima serikali iwe na ustahimilivu wa kulifanyia kazi jambo hili kwa kuangalia pande zote ili kuweza kuongeza mapato