Rais Samia ataja maeneo ya ushirikiano Tanzania, Guinea Bissau

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Guinea Bissau,  zimekubaliana kushirikiana katika kilimo cha korosho, afya, elimu, ulinzi na usalama.

Sambamba na makubaliano hayo, pia nchi hizo mbili zimesaini mkataba wa makubaliano wa ushirikiano katika sekta ya uwekezaji na biashara.

Hiyo yameelezwa leo Jumamosi, Juni 22, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan, alipozungumza na wanahabari baada ya mazungumzo yake ya faragha na Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo aliyewasili nchini kwa ziara ya siku mbili.

Rais Samia amesema kwa kuwa mataifa hayo mawili ni wazalishaji wakubwa wa korosho, hivyo wamekubaliana kushirikiana katika kilimo cha zao hilo.

Ushirikiano huo kwa mujibu wa Rais Samia, ni katika utafiti wa kilimo cha zao hilo na  uchakataji wake ili zipelekwe sokoni zikiwa zimeshaongezewa thamani.

“Kwa kuwa nchi zetu ni wazalishaji wakubwa wa korosho tumeona tuanze kwa kushirikiana kwenye eneo hili, hasa kufanya utafiti na uchakataji wa korosho,” amesema Rais Samia.

Sambamba na ushirikiano huo, maeneo mengine watakayoshirikiana amesema ni katika biashara na uwekezaji.

Ameeleza Afrika kwa sasa ipo mbioni kufungua soko huru, hatua inayotarajia kuongeza viwanda, hivyo ushirikiano ni jambo muhimu ili kuvuna fursa tarajiwa.

Ushirikiano mwingine, amesema utafanyika katika afya, elimu, ulinzi na usalama, utalii na masuala ya fukwe.

“Nchi zetu mbili zina eneo kubwa la mwambao wa pwani na zote zipo katika nafasi nzuri ya kufanya biashara na zinapakana na nchi zisizo na mwambao, tutashirikiana katika hili pia,” amesisitiza.

Hata hivyo, amesema katika mazungumzo yao ya faragha pamoja na mambo mengine,  wamegusia kuhusu maeneo huru ya uwekezaji na kwamba Rais Embalo atatembelea EPZA.

Nchi mbili hizo, Rais Samia amesema zimekubaliana kushirikiana na mataifa mengine kuhakikisha bidhaa zake za mazao ya kilimo zinauzwa kwa bei nzuri.

Mkuu huyo wa nchi, amesema ziara ya Rais Embalo ni mara ya kwanza na kwamba amemwalika naye kwenda kutembelea nchini Guinea Bissau.

Katika hotuba yake, Rais Embalo amesema kuna umuhimu wa mataifa hayo kushirikiana ili kujenga nguvu ya pamoja.

Nguvu ya pamoja, amesema itaiwezesha Afrika kufikia malengo yake ya mwaka 2063 ya kuandaa mustakabali wa dunia.

Kwa kuwa nchi hizo zina historia ya ushirikiano tangu harakati za ukombozi, Rais Embalo amesema ni muhimu hilo liendelezwe.

“Mataifa ya Afrika yakishirikiana yana uwezo wa kuandaa mustakabali wa dunia, kwa kuwa ina rasilimali za kutosha,” amesema.

Ameikaribisha sekta binafsi ya Tanzania kuona fursa zilizopo katika taifa la Guinea Bissau, akidokeza ni lango rahisi la kuzifikia nchi za Magharibi.

“Ni muhimu kubadilisha uhusiano uwe imara zaidi kwani Guinea hawawezi kusahau kuhusu Tanzania na wamekuwa wakifunzwa kuhusu Mwalimu Nyerere shuleni,” ameeleza.

Hata hivyo, ameahidi kuleta wanafunzi mbalimbali kwa ajili ya kujifunza Kiswahili, akisema ndiyo lugha inayoiunganisha Afrika.

Related Posts