Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limesikia kilio cha wazazi na walezi wa wahitimu wa kidato cha sita ambao waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya kwa mujibu wa sheria, lakini hawajaripoti baada kuwaruhusu kwenda kwenye kambi zilizo karibu na makazi yao.
Hivi karibuni Mkuu wa JKT, Meja Jenerali, Rajabu Mabele alitoa wito kwa wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2024 kujiunga na mafunzo ya JKT kwa lazima mwaka 2024.
Vijana hao walitakiwa kuripoti katika kambi walizopangiwa wakiwa na vifaa walivyoainishiwa, kuanzia Juni Mosi, 2024 hadi Juni 7, 2024.
Leo Juni 22, 2024, Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Rajabu Mabena aliwatangazia vijana wote walioitwa katika mafunzo hayo ya lazima lakini hawajaripoti kambini hadi sasa, kuripoti mara moja katika kambi za karibu.
Amesema uamuzi wa kuwataka kuripoti katika makambi yaliyo karibu badala ya yale waliochaguliwa awali, unatokana na jeshi hilo kupokea maombi kutoka kwa wazazi na walezi ya kuomba kubadilishiwa kambi.
Brigedia Jenerali Mabena amesema kwa kawaida vijana wanaenda kusoma katika maeneo tofauti nchini, hivyo kutokana na utaratibu wa kuwapangia kambi zilizopo karibu na shule walizosoma wengine wanajikuta wakilazimika kugharamia nauli kubwa kwenda kuripoti.
“Lakini unaweza kukuta kijana anakwenda kusoma Songea (Ruvuma) lakini yeye anaishi Musoma (Mara). Na wote tunajua hali za kiuchumi. Tumekuwa tukipata simu nyingi sana kutoka kwa wazazi na baadhi ya walezi wakiomba vijana wao kubadilishiwa kambi,” amesema.
Amesema wengi wa vijana waliopangiwa walishindwa kuripoti kwa kukosa nauli na kwa kuwa walezi na wazazi walionyesha changamoto hiyo wakati walipokuwa wakiwapigia simu, JKT imeamua kuwaruhusu kuripoti katika makambi yaliyo jirani.
“Sisi tulizingatia hili ndio maana katika tangazo hili tumewaambia kuwa vijana hawa (wasioripoti hadi sasa), waripoti katika kambi zilizopo karibu yao ,” amesema Brigedia Jenerali Mabena.
“Inawezekana kijana anaishi Arusha lakini alipangiwa kambi iliyoko Rukwa na ameshindwa kusafiri sasa ili apate fursa hii kambi iliyoko karibu na kwake inaweza kuwa Olijoro ama Makuyuni popote pale,” amesema.
Aidha, Brigedia Jenerali Mabena amesema JKT imetoa nyongeza awamu ya pili ya vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka 2024, kujiunga na jeshi hilo ili kufanya mafunzo hayo ya lazima.
Amesema orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo awamu ya pili na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT.
Aidha Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana hao wanatakiwa kuripoti katika kambi za jeshi hilo kuanzia Juni 22, 2024 (leo) hadi Juni 26, 2024.
Zaidi ya wahitimu wa kidato cha sita 52,000 walipata fursa ya mafunzo kwa mujibu wa sheria kwa mwaka jana.