Unyanyapaa bado kikwazo kwa wanaoishi na VVU

Unguja. Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha) na Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar (Zapha+), wameingia makubaliano kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili, ukiwamo unyanyapaa.

Licha ya kuwapo mafanikio katika kukabiliana na watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), wameeleza bado wanakabiliwa na unyanyapaa katika jamii inayowazunguka.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo Juni 22, 2024, Zanzibar Mwenyekiti wa Bodi ya Zapha+ Hasina Hamad Shehe amesema bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili, ambazo kama hawatakuwa na juhudi za pamoja kamwe hawawezi kufanikiwa.

“Unyanyapaa, ubaguzi wa kutisha kwa watu wanaoishi na VVU katika jamii bado upo na unaendelea kutukwaza, katika maeneo mengi ya huduma za kijamii, hospitalini hata shuleni unyanyapaa unaendelea,” amesema.

Amesema ushirikiano utasaidia kwa kiasi kikubwa kutokomeza janga hilo kwani kuna mwingiliano mkubwa wa kijamii na kiuchumi kwa hiyo lazima washirikiane.

Hata hivyo, amesema kuna mabadiliko katika kupambana na janga hilo lakini bado kuna safari ndefu ya kufikia malengo ya dunia ya kuondokana na maambukizi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nacopha, Leticia Kapela amesema hatua hiyo ni ya kihistoria katika taasisi hizo, akieleza itasaidia kutengeneza umoja kufanya kazi kwa pamoja kutokomeza maambukizi.

Amesema kutokana na umoja huo wanayo kila sababu taasisi hizo kuangalia ni jambo gani au shughuli gani watakayoifanya kwa pamoja na Serikali zote mbili kuona umuhimu wa umoja wao.

“Kwa pamoja umoja wetu huu na upendo tuudumishe tuweze kufikia malengo yetu ya kufikia sifuri 3 mwaka 2030,” amesema.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) mwaka 2023, watu 10,580 sawa na asilimia nne ya Wazanzibari 1.8 milioni wanaishi na VVU, kiwango ambacho kinatajwa kuwa kikubwa ikilinganishwa na idadi ya watu nchini.

Related Posts