Ifakara walia na adha ya maji

Ifakara. Wananchi wa kijiji cha Mpanga kilichopo katika halmashauri ya mji wa Ifakara wapo hatarini kupata magonjwa ya kuhara na homa ya matumbo, kutokana na kutumia maji ya kisima yasiyokuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Maji hayo yenye mwonekano wa maziwa yamekuwa yakitumiwa na wananchi wa kijiji hicho hasa wa kitongoji cha Miwangani A kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kunywa na kupikia, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wameeleza namna wanavyopata shida ya maji, hali iliyowafanya wachimbe kisima kifupi cha kienyeji ambacho kinatoa maji meupe mithili ya maziwa maarufu kama “maji ya nzasa” na mara kwa mara wamekuwa wakiugua magonjwa ya tumbo na kuhara.

Mmoja wa wananchi hao, Josephine Mbawala amesema kijiji hicho hakijawahi kupata maji safi ya bomba badala yake wamekuwa wakitumia maji ya visima,  na hivyo ameiomba Serikali kutupa jicho kwenye kijiji hicho na kupeleka huduma ya maji safi na salama.

“Kabla ya kuchimba kisima hiki cha kienyeji mwaka 2000, tuliwahi kuchimbiwa kisima cha kupampu (mdundiko) lakini kwa sasa kisima hicho hakitoi maji ya kutosha kutokana na miundombinu yake kuchakaa maana hata muda wa kupampu inabidi mtu atumie nguvu kubwa ndio apate maji, sasa kuna wakati tunalazimika kuchota maji kwenye kisima hiki cha kienyeji,” amesema Mbawala.

Ameongeza kuwa kisima hicho cha kienyeji, wanachota maji kwa kutumia kata, hivyo ni hatari kwa watoto hasa wanapokwenda kuchota maji na pia muda wote kisima hicho kipo wazi, wadudu na wanyama wengine wanatumbukia.

Naye Clesensia Rashid, mkazi wa kitongoji cha Nyalubungo katika kijiji cha Mpanga, amesema kisima kilichopo cha kupampu hakitoshelezi mahitaji ya wananchi kwa kuwa miundombinu yake imeharibika na hivyo kupoteza uwezo wa kutoa maji mengi.

“Ili kisima hiki kitoe maji mengi, ni lazima utumie nguvu kama unatwanga. Hapa hata watoto tunashindwa kuwatuma kuja kuchota maji, na tunalazimika kutoka nyumbani usiku kuwahi foleni ya kuchota maji ukichelewa unakuta kisima kimekauka au unakuta maji yameshachafuka,” amesema Clensensia.

Diwani wa kata ya Kisawasawa, Songo Daniel amesema ni kweli kijiji hicho kinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama na hivyo wananchi wanajikuta wakitumia maji ya visima vifupi ambayo sio salama kwa afya zao.

Ameeleza mikakati ya Serikali kuwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya maji kupitia Ruwasa ambapo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, Ruwasa imetenga Sh500 milioni kuboresha miundombinu ya maji ikiwemo ujenzi wa visima.

Kupitia mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara unaosimamiwa na RCC kata ya Kisawasawa ni miongoni mwa kata sita zitakazonufaika kuchimbiwa kisima ambapo kwa kata hiyo kisima hicho kitachimbwa kwenye kijiji cha Mpanga ambacho kinakabiliwa zaidi na changamoto ya maji.

“Tayari ujenzi wa kisima hicho umeanza na baada ya kukamilika tunatarajia kuwa na tenki litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhia maji lita 50,000 ambapo naamini changamoto ya maji itakwenda kuisha, hivyo niwaombe wahusika wa mradi huu waweze kuharakisha ili wananchi wapate maji safi na salama,” amesema Daniel.

Related Posts