Ukosefu takwimu halisi za watalii mwiba sekta ya utalii

Unguja. Licha ya sekta ya utalii kupiga hatua na kuchangia asilimia 30 ya Pato la Taifa, bado kuna changamoto ya kupata idadi kamili ya wageni wanaoingia Zanzibar, hivyo kuwapo mianya ya upotevu wa mapato.

Hata hivyo, uzinduzi wa huduma ya mawasiliano ya kipekee kwa watalii ijulikanayo ‘Hakuna Matata’ itakayotolewa na TigoZantel, imetajwa kuwa sehemu ya kutibu tatizo hilo.

Akizindua huduma hiyo leo Juni 22, 2024 Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar, lakini bado inakumbana na changamoto ya takwimu za wageni.

“Kama kuna eneo ambalo tunapata shida kubwa sana katika sekta hii ni katika suala la takwimu, kujua idadi ya wanaoingia, maeneo wanapenda kutembelea, hili ni eneo ambalo bado kama msimamizi wa sekta kuna kazi ya kufanya,” amesema.

Amesema kupata data ambazo ni safi kuonyesha uhalisia wa wageni tangu anapoingia uwanja wa ndege au bandarini ajulikane anaenda katika hoteli, hayo yote yanasaidia kufanya maamuzi na kuweka mipango madhubuti.

Hivyo, Waziri Soraga ameipongeza TigoZantel kubuni mpango huo ambao wageni watasajiliwa wanapofika Zanzibar na kujulikana wanapoenda.

Soraga amesema sekta hiyo ni nyeti na muhimu ukiachilia mbali kuchangia asilimia 30 ya Pato la Taifa, utalii unachangia zaidi ya asilimia 80 ya fedha zote za kigeni na inatoa ajira zaidi ya 200,000 sawa na zaidi ya asilimia 60 ya ajira zote katika mnyororo wa thamani unaotokana na sekta ya utalii.

Ofisa Mkuu wa Biashara TigoZantel, Isaack Nchunda amesema wanaonyesha dhamira ya kuchangia kwenye ajenda ya Serikali ya kuhakikisha watalii wanafurahia vivutio vilivyopo Zanzibar, na wanaendelea kuwasiliana na kubadilishana vivutio hivyo na jamaa zao duniani kwa ujumla kupitia vifurushi vya Jambo Pack.

“Kupitia kampeni ya ‘Hakuna Matata’ tutaingia ubia na hoteli, mamlaka za viwanja vya ndege na migahawa maarufu hapa Zanzibar ili kuhakikisha huduma inawafikia watalii wetu katika maeneo watakayokuwapo hapa visiwani kwa haraka na usalama zaidi,” amesema.

Related Posts