Arusha. Watoto watatu wa familia moja wamepoteza maisha na wengine wanane kunusurika, akiwemo mtoto mchanga wa siku tano katika ajali ya moto iliyotokea eneo la Olmatejoo jijini Arusha.
Chanzo cha moto huo kinatajwa kuwa ni kompyuta mpakato iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme kushika moto na kuunguza kochi na kusababisha vifo vya watoto hao.
Katika tukio hilo, watu wengine wanane wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru jijini Arusha.
Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Jeradi Nonkwe amesema tukio hilo limetokea leo Jumamosi Juni 22, 2024, saa 11 alfajiri.
Amesema chanzo cha vifo hivyo ni watoto hao kuishiwa nguvu baada ya kumeza moshi wa uliotokana na moto uliosababishwa na joto la kompyuta iliyokuwa juu ya kochi huku imechomekwa kwenye umeme.
“Leo asubuhi, saa 11:30 alfajiri, tulipata tukio la moto katika eneo la Olmatejoo na tulipofika tulikuta wasamaria wema wameanza shughuli za uokoaji ambapo tulifanikiwa kuwatoa jumla ya watu 11 kwenye nyumba hiyo,” amesema Nonkwe.
Amesema kati ya watu 11, watu watano walikuwa wako katika hali mbaya, wakiwemo watoto wanne na mtu mzima mmoja.
“Baada ya muda kidogo wa kuwafikisha hospitali, tulipata taarifa watoto watatu kati ya wale wanne waliokuwa katika hali mbaya wamefariki dunia ambao ni Mariam Zuberi (9), Salma Zuberi (7) na Bisma Zuberi (3) huku mtoto mchanga mwenye siku tano akiendelea vizuri,” amesema Kamanda Nonkwe.
Amewataja wengine wanaoendelea na matibabu kuwa ni wazazi wa watoto hao ambao ni Zuberi Msemo (40) na Jasmine Khatibu (33), wanafamilia wengine ni Mariam Mussa (60), Mwanaid Aldina (50), Mussa Msemo (34), AbdulKarim Ramadhan (9) na dada wa kazi aliyefahamika kwa jina moja la Esta (20).
Akizungumzia tukio hilo, Mohamed Mussa (28) ambae ni mwanafamilia, amesema akiwa amelala chumba cha nje alfajiri ya saa 11:30, alisikia kelele akiitwa na kaka yake (baba wa familia) na alipotoka ndio akakutana na moshi mkubwa unatokea ndani kupitia matundu ya madirisha na mlango.
Katika kelele hizo, majirani walitoka na kuanza kutoa msaada wa kuvunja geti la kuingia ndani na baadaye kuanza kuvunja madirisha na kuingia ndani kwa ajili ya kuwatoa kutokana na mlango kukaza.
“Nilifanikiwa kuingia na kuanza kutoa watoto ambao walionekana walianza kupoteza nguvu, pia dada wakubwa na mama yetu kabla ya kusaidiana na majirani kutoa wazazi wa watoto na kuwahishwa Hospitalini” amesema Mohamed.
Mmoja wa madereva bodaboda wa eneo hilo, Ernest Swalehe amesema akiwa anapita katika eneo hilo asubuhi akitokea mjini alikompeleka abiria, aliona nyumba hiyo iliyopo pembezoni mwa barabara ikifuka moshi, ndipo akaanza kuita watu ndani kabla ya kuanza kuamsha majirani wengine.
“Nilipoona kimya na najua hii nyumba huwa ina watu wengi, nilipaki pikipiki na kuanza kugonga mageti ya jirani ambao nao waliitika kwa wingi na kuanza kuvunja geti kabla ya kuingia ndani na kung’oa madirisha, tukafanikiwa kuwatoa watu hao,” amesema Swalehe.