JKU kupewa ndoo ya ubingwa kecho New Amaan Complex

MAAFANDE wa JKU imemaliza ubishi kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada ya kutoka sare ya 1-1 na Kipanga, na kesho jumapili itakabidhiwa taji hilo katika sherehe zitakazoenda sambamba na mechi maalumu itakayopigwa Uwanja wa New Amaan, Unguja.

JKU iliyokuwa ikiongoza msimamo wa Ligi hiyo kwa muda mrefu ilikuwa inahitaji pointi moja tu kabla ya mechi za juzi za kufungia msimu kwani Zimamoto iliyokuwa na pointi 62 ilikuwa na nafasi ya kubeba taji kama ingeshinda mbele ya New City na vinara hao kupoteza.

Hata hivyo, kilichotokea ni kwamba Zimamoto ilikubali kipigo cha mabao 2-0 mbele ya New City na kuirahisishia kazi JKU iliyomaliza msimu na pointi 66 na kutwaa ubingwa huo uliokuwa hauna mwenyewe kutokana na KMKM iliyokuwa ikiushikilia kwa misimu mitatu mfululizo kuutema mapema na kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na alama 57 tu.

Kipigo cha Zimamoto ilichokutana nacho kwenye Uwanja wa Mao B kimeiacha timu hiyo ikisalia nafasi ya pili kwa kukusanya pointi 62, huku Kundemba licha ya kushinda 2-1 dhidi ya Malindi haikuizuia kushuka daraja ikizifuata Ngome, Jamhuri na Maendeleo zilizotangulia.

Kundemba imemaliza na pointi 35, lakini ushindi wa timu za Hard Rock na New City zimeifanya imalize nafasi ya 13 na kukamilisha idadi ya klabu nne zinazopaswa kushuka daraja kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo. 

Hard Rock ilipata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Maendeleo na kufikisha pointi 36, wakati New City iliyoitibulia Zimamoto kwa kuifunga mabao 2-0 ilimaliza na 37 na kuiachia msala Kundemba.

Bingwa mpya wa ZPL atakabidhiwa Kombe leo Jumapili katika mechi maalumu itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan itakayoikitanisha JKU dhidi ya Bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, Muembe Makumbi.

Mgeni Rasmi wa mchezo huo na tukio zima la mabingwa hao kupewa kombe anatrajiwa kuwa, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita na shughuli zitaanza saa 10:00 jioni na mechi ikiisha ndipo JKU utapewa taji hilo la tatu kwao.

Mara ya mwisho kwa timu hiyo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar ilikuwa 2018-2019 ilipotetea kwa msimu wa pili mfululizo, kwani 2017-2018 ililibeba kwa mara ya kwanza.

Related Posts