Utafiti wabaini hatari utumiaji usiofaa wa protini lishe

Dar es Salaam. Utafiti mpya umeonyesha matumizi yasiyo sahihi ya protini lishe za mazoezi, yanaweza kusababisha kuziba ghafla mishipa mikubwa ya damu ya moyo. Hayo ni kwa mujibu wa  Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Chapisho la utafiti huo lililowekwa kwenye jarida la SAGE Open Medical Case Reports la nchini Uingereza, linashabihiana na utafiti mwingine uliofanywa na taasisi hiyo mwaka 2023 kuhusu athari za vinywaji vya kuongeza nguvu maarufu ‘energy drink’.

Mei, mwaka huu, Serikali ilisema imetenga Sh3.5 bilioni katika bajeti ya mwaka 2024/25 kwa ajili ya utafiti katika maeneo sita, ikiwemo matumizi ya vinywaji vya kuongeza nguvu.

Akizungumzia chapisho hilo, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti JKCI, Dk Pedro Palangyo amesema mapema mwaka huu katika taasisi hiyo kulitokea tukio ambalo ni nadra kwa Afrika na duniani likihusu protini lishe iliyo katika mfumo wa poda, inayotumiwa zaidi na watu wanaofanya mazoezi.

Dk Palangyo amesema lengo la protini ni kumpa mtu nguvu wakati wa mazoezi ili asichoke na aweze kufanya mazoezi kwa muda mrefu na pia kujenga misuli.

Amesema nchini zilianza kuingia na kutumika miaka michache iliyopita na sasa matumizi yameongezeka.

“Hivi sasa tunaripoti kisa cha kijana wa miaka 25 aliyekuja Taasisi ya Moyo akiwa na maumivu makali ya kifua upande wake wa kushoto, alipofanyiwa vipimo vya awali vya ECO na ECG alionyesha picha ya mishipa ya moyo kuziba,” amesema.

Amesema alipelekwa kwa dharura kuzibuliwa na akiwa katika matibabu uchunguzi ulibaini mshipa mmoja wa moyo kati ya mitatu ulikuwa umeziba kwa asilimia 100.

Dk Palangyo amesema alizibuliwa na kuwekewa kifaa maalumu, baadaye akapelekwa chumba cha uangalizi wa karibu (ICU) kwa siku tatu na baadaye alipona na kurudi nyumbani.

Amesema kupitia kifaa alichowekwa atatumia dawa ili kuhakikisha damu haigandi.

“Siyo kwamba kijana huyu alikuwa anatumia lishe hizi vibaya, lakini siku tatu kabla ya tukio alibadilisha matumizi aliyoshauriwa. Inashauriwa kuchanganya lishe hiyo na maji kutengeneza kimiminika, ndipo unywe au kuchanganya na maziwa ambayo yanatokana na mimea na si ya wanyama,” amesema.

Dk Palagyo amesema katika historia ya mgonjwa, kupitia kundi la WhatsApp la wanamazoezi wenzake ilitumwa video iliyotoka nchi za nje, iliyoonyesha mtu akila lishe kwa kumimina mdomoni.

Amesema kwa kuitumia namna hiyo inaingia moja kwa moja kwenye damu na kumpa nguvu ya haraka zaidi mtumiaji badala ya kuchanganya na maji.

“Katika kisa hiki tunajifunza matumizi ambayo hayajashauriwa na watengenezaji wa lishe hizi, yanaweza kuleta madhara makubwa na hata kifo,” amesema.

“Kijana alikuwa na bahati kwa kuwa alikuwa jijini Dar es Salaam karibu na JKCI, angekuwa sehemu nyingine angepoteza maisha. Ni vizuri jamii ifahamu matumizi ya hivi vitu kwa usahihi, tulianza na energy drink na sasa watu wanakuja kwenye lishe poda,” amesema.

Wataalamu wa mazoezi wameelezea wanamichezo wengi nchini wamekuwa wakitumia lishe hiyo.

Dk Sameer Jamwal, mtaalamu katika Idara ya Biokemia katika Chuo cha Matibabu cha Dk Rajendra Prasad, Kangra cha nchini India alikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akisema: “Kama una uzito wa kilo 50, hakuna tatizo ukitumia gramu 50 za protini kwa siku.”

Mtaalamu wa tiba ya michezo na mwalimu wa mazoezi kutoka ACSM, Waziri Ndonde amesema baadhi ya lishe hizo zipo kwenye orodha ya matumizi ya dawa zilizokatazwa michezoni.

Amesema elimu ni jambo la msingi, kufuata masharti na ushauri juu ya matumizi.

Ameeleza mazoezi yanapofanyika baadhi ya tishu za misuli zinapondwa hivyo kusababisha mwili kupata maumivu, kwa hiyo kazi ya protini hizo ni kurekebisha na kuunda misuli upya.

Ndonde amesema kuna vyanzo vingi vya protini kwenye lishe kama vile ulaji wa nyama na bidhaa zake, kuku na bidhaa zake, mikundekunde, samaki, maziwa, karanga na jamii zake kama vile korosho na vyakula vinginevyo.

“Mwanamichezo anahitaji kiasi cha kati ya gramu 0.93 hadi gramu moja kwa kila kilo ya uzito wake. Kwa mfano mwanamichezo mwenye uzito wa kilo 75 atatakiwa ale (75kg X 0.94 = 70) huyu atatakiwa ale gramu 70 katika kila mlo wake,” amesema.

Hata hivyo, amesema mahitaji ya protini yanapokuwa makubwa, wengine huanza kula virutubisho lishe kufidia kiasi cha protini kwenye mwili kinachohitajika.

“Pamoja na matumizi haya ya protini ya ziada, lazima mwanamichezo awe anapewa lishe kutokana na ushauri wa kitaalamu ili kufidia kwa usahihi. Mchezaji atapimwa damu au mkojo ili kupata kiwango cha mahitaji ya kiasi cha ziada,” amesema.

Ndonde amesema matumizi hayo yakifanywa holela huleta madhara mengi.

“Virutubisho vyote huwa vinasafirishwa na damu kwenda kwenye sehemu za mwili. Kwa maana hii matatizo ya mishipa ya damu na moyo pamoja na figo ni rahisi sana kuyapata,” amesema.

Mtaalamu wa fiziolojia ya homoni na mazoezi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayanshi Shirikishi (Muhas), Dk Fredrick Mashili amesema lishe hizo hazina shida zikitumiwa inavyotakiwa.

“Hazina shida ila ni jinsi watu wanavyotumia wanachanganya, wanabwia bila kuchanganya na maji na haitakiwi kufanya hivyo,” amesema.

Related Posts