KUNA vitu Tanzania vinachekesha sana. Ni kama hili sakata la mchezaji Lameck Lawi, Simba na Coastal Union. Ni kichekesho.
Kwa mara ya kwanza nimeona duniani timu inatangaza kuwa imemnunua mchezaji fulani halafu wale waliomuuza wanakataa.
Yaani, Simba inasema imemnunua Lawi kutoka Coastal Union ya Tanga. Saa chache baadaye Wagosi wa Kaya wanasema hawajamalizana na Simba. Kwamba Simba haikukamilisha taratibu kwa wakati.
Sasa unajiuliza kama Coastal hawajamuuza kwenda Simba, wana ulazima gani wa kupiga kelele mtandaoni? Mchezaji si wa kwao. Wasubiri muda wa kuanza Kambi ukifika aripoti kambini.
Hizi kelele za mitandaoni na makanusho mengi ni ishara kuwa kuna kitu hakipo sawa mahali.
Mtu mmoja ananiibia siri kuwa Coastal imepokea ofa kutoka Ubelgiji hivyo inataka kumuuza huko. Ni ofa kubwa kuliko ya Simba.
Lakini, hata hivyo Simba walikua wameshalipa fedha zote za makubaliano. Tatizo walichelewesha malipo ya awamu ya mwisho kidogo. Hivyo Coastal wanataka kutumia udhaifu huo kuvunja mkataba. Kwa hakika hiki ni kituko kingine cha soka la Tanzania.