Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, kwa mara nyingine akiigusa ofisi yake.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka leo Juni 22, 2024, Rais Samia amewapangia kazi nyingine watumishi wawili waliokuwa maofisa waandamizi, Ofisi ya Rais Ikulu.
Katika taarifa hiyo iliyotiwa saini na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, maofisa hao wameteuliwa kuwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri.
Katika uteuzi huo, Rais Samia amemteua Hassan Mnyika kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo. Kabla ya uteuzi, alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu.
Mnyika anachukua nafasi ya Lain Kamendu ambaye amestaafu.
Pia, amemteua Addo Missama kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi. Kabla ya uteuzi, alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais Ikulu.
Missama anachukua nafasi ya Joseph Mafuru ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Taarifa imesema Rais amemteua Dk Ashura Katunzi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), akichukua nafasi ya Dk Athuman Ngenya ambaye amemaliza muda wake.
Kabla ya uteuzi, Dk Katunzi alikuwa Ofisa Udhibiti Ubora Mkuu wa shirika hilo.