WAKATI viongozi wa Simba wakihaha kukisuka upya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, tayari wameanza kumpigia hesabu winga raia wa Ivory Coast, D’Avila Messi Kessie ambaye inaelezwa huenda mambo yakienda sawa atajiunga na miamba hiyo.
D’Avila kwa sasa anakipiga Inova Sporting Club Association ya Ivory Coast, huku nyota huyo akisifika kwa uwezo wa kucheza winga zote yaani kulia na kushoto ambapo msimu uliopita alifunga mabao 11 na kuasisti sita na kama akitua ataungana na Kramo Aubin aliyesajiliwa msimu uliopita, lakini hakutumika kwa sababu ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu, japo kwa sasa amepona kabisa.
KIUNGO mshambuliaji Mcameroon, Moubarack Amza yupo katika hatua za mwisho kukamilisha dili la kutua kwa mkopo Dodoma Jiji akitokea Singida Black Stars (zamani Ihefu). Nyota huyo aliyewahi kuzichezea Coastal Union na Kagera Sugar inaelezwa dili lipo pazuri na huenda msimu ujao akafanya kazi na Mecky Mexime kwa mara nyingine.
PAMBA Jiji imeanza mazungumzo ya kumnasa winga wa Tabora United Mganda, Ben Nakibinge kwa ajili ya msimu ujao. Nyota huyo amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo iliyoepuka janga la kushuka daraja japo viongozi wa Pamba wanamhitaji ili akaungane na kocha Mserbia, Goran Kopunovic kukisaidia kikosi hicho msimu ujao.
MABOSI wa Dodoma Jiji wameanza mazungumzo ya kumsajili beki wa kulia wa Kagera Sugar, Dickson Mhilu kwa ajili ya msimu ujao. Dodoma inahitaji saini ya beki huyo aliyekuwa katika kiwango kizuri ili akaungane na aliyekuwa kocha wa zamani aliyeifundisha Kagera Sugar, Mecky Maxime aliyetangazwa kukinoa kikosi hicho.
BEKI wa kati wa Tabora United, Mcongomani Andy Bikoko Lobuka amezichonganisha Singida Black Stars na Pamba Jiji zinazomhitaji. Nyota huyo aliyejiunga na Tabora msimu uliopita akitokea SM Sanga Balende, awali alikuwa anaonekana wazi yupo katika nafasi nzuri ya kutua Singida, kabla ya Pamba kuingilia dili ili kuinasa saini yake.
YANGA imeanza mazungumzo ya kumpata kiungo mshambuliaji Mcongoman, Karim Kimvuidi anayecheza Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Nyota huyo (22), ana uwezo pia wa kucheza winga ya kulia na kushoto hivyo kuwavutia viongozi wa kikosi hicho tangu akikipiga Maritzburg Utd ya Sauzi na DC Motema Pembe.
KAGERA Sugar, imeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya beki wa kushoto wa kikosi hicho Mganda, Dissan Galiwango. Hata hivyo, inaelezwa wakati Kagera Sugar ikianza mazungumzo hayo ila mchezaji huyo ameonyesha nia ya kutaka kuondoka kurudi Vipers ya Uganda aliyokuwa akiichezea kabla.
MASHUJAA imeanza mazungumzo ya kumwongezea mkataba mpya beki wao wa kati, Ibrahim Ame kwa ajili ya msimu ujao. Mabosi wa kikosi hicho wanaamini bado nyota huyo ana uwezo mkubwa wa kuwasaidia msimu ujao hivyo kuanza naye mazungumzo na nyota huyo wa zamani wa Coastal Union.