Simba yafuata kiungo Mashujaa | Mwanaspoti

WAKATI fagio likiendelea kutembezwa Simba, mabosi wa klabu hiyo wapo bize kuingiza majembe mapya, kwani baada ya beki Lameck Lawi, tayari imemvuta kiungo mwingine fundi kutoka Mashujaa.

Simba imemsajili kiungo huyo, Omary Omary ikielezwa kashapewa mkataba wa miaka miwili na kilichobaki ni kutangazwa kama ilivyokuwa kwa Lawi aliyenyakuliwa kutoka Coastal Union iliyoamua kuikataa biashara hiyo na Wekundu hao, ingawa inaelezwa kitasa hicho kitacheza.

Inadaiwa Omary aliyewahi kukipiga Tanzania Prisons kabla ya Mashujaa kumchukua na msimu uliomalizika hivi karibuni aling’ara wakati timu hiyo ikipambana na kumaliza nafasi ya nane licha ya awali kuonekana kama ingerudi kule ilipotoka Ligi ya Championship.

Usajili wa kiungo huyo inaelezwa umezingatia suala la umri, kwani mabosi wa Msimbazi wanataka wachezaji wenye umri usiozidi 28 na Omar kwa sasa ana miaka 21 tu na inaelezwa pande zote mbili zimeafikiana na kilichobaki ni kutambulishwa tu.

Kiungo huyo anapotua Simba atakwenda kucheza eneo la kiungo cha Simba chenye nyota kama Fabrice Ngoma, Yusuf Kagoma aliyenaswa pia hivi karibuni kutoka Singida FG , Mzamiru Yasin, Clatous Chama anayetajwa yupo mbioni kutua Yanga na Sadio Kanoute.

Hakuna kiongozi wa Simba aliyethibitisha taarifa hizo, lakini rafiki wa karibu wa mchezaji huyo aliyecheza wote Mashujaa (jina tunalo) alikiri Omary kumalizana na Simba na kudokeza dili lilianza tangu mwanzoni mwa msimu uliomalizika Mei 28 mwaka huu.

“Dili hilo lilikuwa ni suala la muda tu kwani mchezaji huyo alifuatwa kwa mazungumzo akiwa amebakiza miezi sita kuitumikia Mashujaa, hivi ninavyokwambia tayari amemalizana na Simba ili kuitumikia kwa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti lilipomtafuta Omary, alisema ni kweli kwa sasa yeye ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Mashujaa na alipoulizwa juu ya ofa ya Simba, alidai hawezi kulizungumzia  hilo kwani hilo ni jukumu la meneja anayemsimamia.

“Siwezi kuzungumzia ishu ya timu yoyote iliyonifuata kwa mazungumzo kwa sasa kwani,  sio kazi yangu. Meneja ndiye anashughulikia hilo naye ndio anaweza kuweka wazi ni timu gani imeonyesha nia na ipo tayari kunisainisha kwaajili ya kuitumikia msimu ujao,” alisema Omary na kuongeza;

“Ngoja tusubiri mtajua msimu ujao ninacheza wapi.”

Hata hivyo, Msemaji wa Mashujaa, Khamis Malyango alipoulizwa jana juu ya ishu ya Omary alisema klabu haijapata taarifa rasmi, huku akisema Omary bado ni mchezaji wa Mashujaa kwa vile amebakiza mkataba wa miezi sita.

“Tunasikia hizo taarifa kuwa Omary Omary amesaini klabu nyingine, ila kwetu bado hazijatufikia rasmi, tutamtafuta mchezaji kujua ukweli kwani yeye bado ni mchezaji wetu halali amebakiza miezi sita,” alisema Malyango huku akiongeza.

“Mchezaji mwenye mkataba anatakiwa kuheshimu hilo, Mashujaa hatuna shida ya kumzuia mchezaji kuondoka kama pande tatu kwa maana ya sisi, klabu inayomtaka na mchezaji  tutaridhiana, lakini klabu ikifanya mambo kihuni tutakuwa na majibu mazuri dhidi yao.”

Mbali na Omary, Lawi na Kagoma ambao ni wazawa, Simba pia imehusishwa na kumsainisha Joshua Mutale kutoka Zambia na beki Tra Bi Tra kutoka Ivory Coast.

Related Posts