SAGA la usajili wa fundi wa aliyemaliza mkataba wake Simba, Clatous Chama limechukua sura mpya, baada ya bosi mmoja wa Zambia kuvujisha siri kiungo huyo tayari amesaini mkataba wa mwaka moja Yanga.
Ingawa sio Chama wala Yanga waliothibitisha juu ya dili hili, lakini taarifa za ndani kutoka Yanga ni kiungo huyo atakuwa mali ya kikosi hicho kwa msimu ujao.
Utamu zaidi ni kigogo mmoja mzito anayefanya biashara ya kuuza kopa (shaba), alitaka kuvunja Benki kumrudisha Chama Zambia ili kuichezea klabu yake anayoifadhili iliyopo Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Alichofanya bosi huyo ni kutoa kazi kwa wakala mmoja mkubwa ili amdake fasta baada ya kujiridhisha amemaliza mkataba na Wekundu wa Msimbazi hao, lakini akakutana na jibu lililomduwaza kutoka kwa kiungo huyo aliyehusika na mabao 14 msimu uliopita.
Hata hivyo, mara baada wakala huyo kujifungia na Chama wakizungumzia dili hilo, kiungo huyo alishindwa kukubaliana na ofa hiyo akiwaambia atabaki Tanzania, ingawa anaweza kucheza timu tofauti na Simba.
“Alijibu zaidi kuwa atakuja Tanzania hivi karibuni kumalizia tu huo mchakato na angependa kuja kucheza, huku Zambia ni nyumbani lakini kwa sasa anataka kubaki huko (Tanzania) kwa mwaka zaidi,” alisema bosi huyo.
KIGOGO YANGA AFUTA POST YA CHAMA
Wakati Zambia kukiongeza uvumi huo wa Chama kutua Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja, hapa nchini kigogo mmoja mzito ameshtua zaidi baada ya bosi huyo kufuta posti ya kumkashifu kiungo huyo.
Baada ya mchezo kati ya Simba na Yanga kisha Chama kumkanyaga vibaya beki na nahodha msaidizi wa Mabingwa hao Dickson Job, kigogo huyo alipost kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii akionyesha kukerwa na kile ali-chofanya Mzambia huyo.
Baada ya muda mrefu kupita kigogo huyo alifuta post hiyo kwenye ukurasa wake na baadaye alipotafutwa na Mwanaspoti alisema kifupi: “Nimefuta kwa sababu nimemsamehe Chama,” alijibu bosi hiyo huku akicheka mwishoni.