Moshi. Dereva wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Alphonce Edson (54), anatarajiwa kuzikwa kesho Jumatatu, Juni 24, 2024, nyumbani kwake, Kata ya Kahe Magharibi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Edson na aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa (RAS) wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda (56) aliyezikwa jana, mkoani Songwe, walifariki dunia kwa ajali ya gari ilitokea Juni 18, 2024, saa 8:30 mchana, eneo la Njia panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Edson atazikwa nyumbani kwake Kahe na baada ya maziko familia itaupeleka msiba nyumbani Rungwe, mkoani Mbeya.
“Tumezungumza na familia yake, dereva kwao ni Mbeya, lakini kwa vile alikuja Kilimanjaro tangu akiwa mdogo na wazazi wake walimuacha huku ambako ni mwenyeji sana kule Chekereni Mabogini, hivyo familia wameamua kumzika hapo Jumatatu (kesho) na baada ya maziko familia umeomba tupeleke msiba kule nyumbani Rungwe, Mbeya. Sisi tutafanya hivyo, tutatoa gari,” amesema Babu.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi wa Kilimanjaro kuendelee kushirikiana kama walivyofanya kwenye msiba wa RAS huyo na huo pia waonyeshe ushirikiano ule ule. “Tujumuike pamoja twende tukampumzishe mwenzetu,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Akizungumzia utaratibu wa mazishi, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya mazishi, amesema zimekamilika na mwili wa marehemu utatolewa Hospitali ya Rufaa ya KCMC saa 2:00 asubuhi na kupelekwa nyumbani kwake Kahe kwa taratibu za maziko.
“Kwa mujibu wa ratiba, mwili utatolewa KCMC saa 2:00 asubuhi, utapelekwa nyumbani kwake Kahe, kisha itaendelea ratiba ya kuaga na ibada, kabla ya kuelekea makaburini,” amesema Sumaye.