Dar, Pwani zakosa maji kwa saa 48

Dar es Salaam. Wakati wakazi jijini hapa na Pwani wakieleza maumivu wanayopitia kwa kukosa maji kwa zaidi ya saa 48, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imesema tatizo limekwisha na huduma imerejea tangu saa tatu asubuhi leo Jumapili, Juni 23, 2024.

Katika maeneo mengi ya Dar es Salaam na Pwani, wakazi walikosa maji tangu Ijumaa, huku leo Jumapili Dawasa ikitoa taarifa kwa wananchi wanaohudumiwa na mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Juu na Ruvu Chini kukosa huduma hiyo.

Taarifa ya Dawasa imesema, kuna matengenezo ya umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenye mitambo hiyo tangu Jumamosi ya Juni 22, ambayo imesababisha ukosefu wa huduma ya maji kwenye maeneo mengi ya Pwani na Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro amesema huduma ya maji imerejea leo Jumapili saa 3 asubuhi.

“Tayari mitambo imewashwa na huduma ya maji imerejea,” amesema Everlasting na kutolea ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu ucheleweshwaji wa taarifa hiyo, wengi wakidai imetolewa wakati tayari maji yakiwa yamekatwa.

Hata hivyo, Everlasting amedai taarifa ilitolewa Alhamisi ya Juni 20 na matengenezo yalianza Ijumaa.

“Siku hiyo matengenezo hayakumalizika, yaliendelea hadi Jumamosi, tulitarajia siku hiyo yafanyike ndani ya saa hayakumalizika ndani ya muda ndiyo sababu tukatoa taarifa kwa mara ya pili,” amesema.

Amedai, tayari yamekamilika na mitambo imewashwa tangu saa 3 asubuhi leo Juni 23, ingawa baadhi ya maeneo ya Kibaha na Tabata wananchi wengi wamedai hadi saa 5:30 asubuhi hayakuwa na maji.

Matlida Joseph wa Kibaha kwa Mathias amesema tangu Alhamisi maji yalikatika hadi sasa (ilikuwa saa 6 mchana) hawana maji kwa zaidi ya saa 48.

“Wenye uwezo walikuwa wakinunua ya madumu, sisi wa chini tumelazimika kutumia maji ya chemchem yaliyotokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni, maeneo mengi kama si yote ya Kwa Mathias hayakuwa na maji tangu Alhamisi,” amesema.

Mkazi wa Kibaha Kongowe, Fatma Ramadhan amesema wameingia gharama kununua maji ya madumu kwa wauzaji maji baada ya kukosekana huduma ya maji ya Dawasa kwa zaidi ya siku mbili.

“Binafsi sikujua kama walitoa tangazo la kukatika maji, hadi leo Jumapili, kama wangekuwa wanafanya ukarabati basi wawe wanatoa taarifa hata wiki moja kabla ili tujipange,” amesema.

Mbali na Kibaha, pia maeneo mengi ya Dar es Salaam huduma hiyo ilikosekana huku wakazi wa Kimara King’ongo na Tabata nao wakilalamika kukosa huduma ya maji kwa muda mrefu hata kabla ya tangazo la Dawasa.

“Ni zaidi ya wiki moja sasa Tabata hatuna maji, tangazo la Dawasa limekuja tayari kwetu hatua maji, tunalazimika kutumia maji chumvi muda wote,” anasema Devotha Juma.

Mkazi wa King’ongo, Mussa Jumanne amesema tangazo la Dawasa limekuja tayari wao wakiwa hawana maji takribani siku tatu.

“Hivi sasa tumeshazoea kutumia maji ya chumvi, tunanunua dumu 300, siku tukikumbukwa na Dawasa tunashukuru, lakini kwenye maji huku kwetu ni changamoto,” amesema.

Related Posts