Dodoma. Hatima ya maumivu au unafuu wa maisha kwa Watanzania, itaamuliwa na wabunge wiki ijayo wanapokwenda kupiga kura ya kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Sambamba na hilo, wiki ijayo itaamuliwa hatima ya tuhuma za kudharau mamlaka ya Spika na Bunge zinazomkabili Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina.
Juni 13, 2024, Serikali ilipendekeza kukusanya na kutumia Sh49.3 trilioni, ikiwa ni bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25, huku hoja mbalimbali zikiibuliwa na wabunge na wadau wakigusa maeneo yanayoumiza wananchi.
Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa ipo inayohusu sheria mpya ya kodi ya Sh382 kwa kilo moja ya gesi ya magari, ambayo baadhi ya wabunge wameonyesha kuipinga.
Hoja nyingine ni sakata la bei ya sukari kupanda kila mwaka, kikokotoo, madeni ya Serikali kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, watu kujificha kwenye kauli ya ‘mama anaupiga mwingi’ na matumizi ya malipo kwa mfumo wa kidigitali.
Kama hiyo haitoshi, ugumu wa upatikaji dola ya Marekani na jinsi ya kupunguza matumizi ya fedha hizo, madeni ya wakandarasi wa ndani na nje ni baadhi ya hoja nyingine.
Hoja zote hizo zinawasubiri Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kuzipatia majibu, kisha upitishaji wa bajeti hiyo uendelee.
Baada ya kuhitimisha wabunge watapiga kura kwa utaratibu wa kuitwa mbunge mmoja mmoja kwa jina na kuulizwa iwapo anaunga mkono ama la, kisha kuhesabiwa kwa kura zitazotoa uamuzi kuhusu bajeti hiyo. Hili litafanyika Jumatano ya Juni 26, 2024.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 23, 2024, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema wabunge wengi wametimiza wajibu wao kwa kutetea wananchi na majimbo yao katika mjadala wa bajeti.
Amesema wamegusa maeneo ambayo ni changamoto kwa wananchi, ikiwemo barabara za vijijini ambapo vipaumbele vya kuzijenga vipo, lakini kutokana na uhaba wa fedha wakukidhi mahitaji yote.
Amesema katika mijadala ya bajeti hiyo, pia wameona wabunge wengi wakizungumzia umuhimu wa baadhi ya mabadiliko ya kisera yanavyoweza kulinda viwanda vya ndani ikiwemo eneo la sukari.
“Ni dhahiri Serikali haiwezi kuacha wadau wake, imefafanuliwa mara kadhaa na Waziri wa Kilimo kuwa walaji na viwanda vinalindwa. Takwa la Serikali halipishani sana na mahitaji ya wabunge sema tu uhaba wa rasilimali ambayo ni changamoto ya kila mwaka,” amesema Mwinuka ambaye ni mchumi kitaaluma.
Najim Hamad, mkazi wa Kimara Dar es Salaam, ameeleza kilichobaki ni uamuzi wa kupitisha au kutopitisha kwa kuwa hoja zilizoibuliwa zimejitosheleza.
Hamad anayejishughulisha na udereva wa teksi mtandao, amesema amesikia maoni na hoja za wabunge kuhusu kodi kwenye gesi zinazotumika katika magari na kwamba ameridhishwa nayo.
Lakini, amesema kinachosubiriwa ni uamuzi wa kuipitisha sheria hiyo au kuibatilisha kutokana na hoja zilizoibuliwa.
“Wabunge siwadai chochote, wameeleza vizuri, ile kodi inatuumiza hasa sisi tunaofanya biashara hizi (teksi mtandao), tunasubirikwa hamu uamuzi utakaofikiwa,” amesema.
Hoja ya kubana matumizi ya Serikali, ndiyo uamuzi unayosubiriwa na Delta Maziku kutoka bungeni wakati wa upitishaji wa bajeti hiyo.
“Ni maamuzi haswa kwa sababu yale yote yaliyosemwa na wabunge yanakwenda kuamuliwa sasa ndani ya bajeti hiyo,” amesema.
Mpina naye atajua hatima yake
Kesho Jumatatu Juni 24,2024 itakuwa siku ya kuwasilishwa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Haki Kinga na Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu tuhuma zinazomkabili Mpina za kudharau mamlaka ya Spika na Bunge kwa Spika Dk Tulia Ackson.
Yawezekana baada ya kuwasilishwa kwa Spika Tulia akiwekwa kwenye mpango wa kusomwa taarifa bungeni kesho ama siku yoyote kati ya kesho hadi Ijumaa ya Juni 28, 2024, siku ambayo mkutano wa Bunge utaahirishwa.
Pia kamati hiyo itawasilisha taarifa ya walichokiona katika ushahidi wa Mpina kuhusu tuhuma alizozitoa kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwamba alisema uongo bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha Juni 4, mwaka 2024.
Taarifa hiyo inatokana na uamuzi wa kumpeleka katika kamati hiyo uliotolewa Juni 18, 2024 na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliyesema kupeleka ushahidi alioamuagiza kwenye vyombo vya habari ni kudharau mamlaka ya Spika.
Dk Tulia alisema pia kitendo hicho ni kuingilia mwenendo wa Bunge na kushusha hadhi na heshima ya Bunge.
Pia, Spika amezipeleka kwenye kamati hiyo nyaraka za ushahidi wa Mpina dhidi ya Waziri wa Kilimo, Bashe kwamba amelidanganya Bunge kuhusu utoaji wa vibali vya kuingiza sukari nchini.
Dk Tulia alisema ni dhahiri kitendo cha Mpina kuwasilisha nyaraka za ushahidi kwa Spika na wakati huohuo kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu maudhui ya nyaraka hizo ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa Bunge na Spika.
“Kifungu cha 26 (d) cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, sura 296 kinazuia kitendo cha kumkosea heshima Spika.
“Kifungo cha 26 (e) kinazuia vitendo vya dharau kwa mwenendo wa shughuli za Bunge, aidha kifungu cha 34, kifungu kidogo cha kwanza (g) kinazuia kuchapisha kwa umma taarifa zilizoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni pasipo kupata kibali cha Bunge na kabla ya taarifa hizo kuwekwa mezani.
“Kitendo cha Mpina kinakwenda kinyume na kifungu cha 29 (d na e) na kifungu cha 34, kifungu kidogo cha kwanza (g) vya sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge sura 296.
Akizungumzia adhabu hizo, Wakili Elias Machibya amesema kupewa adhabu ya kufungiwa kunawaathiri pia wapigakura kwa kukosa uwakilishi pindi mbunge huyo anapozuiwa kuingia katika vikao vya Bunge.
“Wananchi wakikosa uwakilishi ina maana wanakosa sauti ya kuwasemea, lakini mtu ambaye ni mbunge anatakiwa kuwa na tabia ambazo ni kielelezo kwa jamii kwa sababu ni kiongozi wa kitaifa,” amesema.
Amesema hivyo inapasa mbunge kujitunza kwa kujua kuwa ana dhamana sio tu kwa wapigakura wake, bali ya Bunge pia.
“Kanuni za Bunge zinachukua mkondo wake kwa mtu yoyote akionyesha tabia isiyofaa, ili kulinda hadhi na heshima ya Bunge…Kwa Spika asiposimamia vizuri sheria anaweza kufanya Bunge kushusha hadhi kwa jamii,” amesema.
Machibya amesema hakuna namna ya kulegeza adhabu hizo kwa kwa sababu watashusha hadhi ya Bunge, hivyo ni jukumu la wabunge kukaa sawa kimaadili, ili kulinda hadhi na heshima ya Bunge kwa ajili ya maslahi ya Taifa na wapigakura wake.
Iwapo Mpina atakumbana na aina yoyote ya kibano kutoka kwa kamati hiyo, kuna uwezekano akabanwa pia na chama chake ambacho awali Kamati ya Maadili ya CCM Wilaya ya Meatu ilishamhoji.
Atakapohukumiwa kwa kudharau mamlaka ya Spika na kulidharau Bunge, maana yake amezidharau mamlaka ambazo CCM inaziheshimu na hivyo dharau hizo zitaamua kuadhibiwa ndani ya chama chake.
Adhabu zinazowezekana kwa mbunge huyo kwa mujibu wa kanuni za maadili za chama hicho ni kupewa karipio, kuonywa na asipojirekebisha ndani ya kipindi cha adhabu atafukuzwa uanachama.
Waliowahi kubanwa na kamati
Baadhi ya wabunge waliowahi kukutana na kibano cha Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ni Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Saed Kubenea (Ubungo), James Ole Miliya (Simanjiro) na Suzan Lyimo na Anatropia (Viti Maalumu), wote walikuwa Chadema.
Wengine ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini), Conchesta Rwamlaza (Viti Maalum), Jesca Kishoa (Viti Maalum), pia walitokana na Chadema.
Kwa upande wa CCM, Josephat Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga), Stephen Masele (aliyekuwa mbunge wa Shinyanga Mjini).
Halima Mdee na Ester Bulaya (Viti Maalumu) nao waliwahi kupewa adhabu ya kufungiwa kutohudhuria Bunge mikutano minne (mwaka mmoja) baada ya mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Wabunge hao walituhumiwa kudharau mamlaka ya spika kwa kukaidi maelekezo yake ya kuwataka watulie, ili Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliyepewa nafasi ya kuzungumza aendelee.
Hata hivyo, kamati hiyo iliwahi kutoa msamaha kwa aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kwa kosa la kudharau mamlaka ya Spika, ikiwemo kupiga kelele bungeni na kutupa karatasi ovyo.