Unguja. Sheikh Said Nyange (48) amefariki dunia baada ya kuugua ghafla akiwa Makka nchini Saudi Arabia alipokwenda kuhiji.
Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumapili, Juni 23, 2024 Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Juwaza), Muhidin Zebeir Muhidin amesema kiongozi huyo amefarikia dunia usiku wa kuamkia leo huko Saudia.
“Ni kweli sheikh Said Nyange amepoteza maisha usiku wa leo na tayari ameshazikwa hukohuko baada ya kupata ridhaa kutoka kwa familia,” amesema.
Kwa mujibu wa Katibu Muhidin, Sheikh Nyange aliugua ghafla Juni 18 na kukimbizwa hospitali kabla ya kufarikia dunia jana Juni 22, 2024.
Sheikh Nyange mbali ya kiongozi wa dini, pia alikuwa ni Sheha wa Shehia ya Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa mujibu wa Katibu Muhidini, Sheikh Nyange alipokuwa Makka alikuwa akiendelea kuwaongoza mahujaji katika maeneo mbalimbali.
“Tumepokea kwa masikitiko makubwa, alikuwa kiongozi hodari mnyenyekevu kwa kila mtu,” amesema.
Sheikh Nyange ameacha wajane watatu na watoto tisa.