NaCoNGO yalia na kodi, ada za kila mwaka

Dodoma. Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), limeiangukia Serikali kushughulikia changamoto ya mashirika ya kiserikali ikiwamo kuchukuliwa kama sekta binafsi.

Akizungumza leo Jumapili Juni 23, 2024 mjumbe wa kamati ya mpito ya uchaguzi wa NaCoNGO, Dk Astronaut Bagile amesema leo watajadili pia ni jinsi gani wanaweza kuwa na nguvu ya ushawishi kwenye masuala yanayotatiza shughuli zao.

Amesema kwa mfano suala la kupata vibali vya msamaha wa kodi ili wasitozwe kwa kuwa mashirika hayo hayafanyi biashara, lakini kuna sheria mbalimbali za kodi ambazo kwao ni kikwazo.

“Kwa mfano ikifika mwisho wa mwaka unatakiwa uwe na 0 balance ukienda mwaka wa pili ukiwa na balance unatakiwa kulipa, kwa kuwa sisi tunakuwa treated (kushughulika) kama private sector (sekta binafsi).

“Baraza linalokuja jipya lazima lishughulike na hizo changamoto, kwa mambo ambayo yana tatizo katika utekelezaji shughuli zozote na kuwasilisha serikalini kwa utekelezaji,” amesema.

Amesema sheria inahitaji mapitio ambayo yatakuwa na mambo mengi ya kuyaangalia wakati mchakato utakapoanza.

“Kwa hiyo rai imetolewa kusitolewe penati kama wote tunafanana, lakini iangalie makundi maalumu na changamoto walizonazo na namna gani wanaweza kuwatazama kwa jicho lingine ili waweze kutimiza majukumu yao,” amesema Dk Bagile.

Naye, Mratibu wa mafunzo hayo, Ntimi Charles amesema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali hata kama wamepata usajili ni lazima yawe na uhalali kwa wanachokifanya kwenye jamii.

“Wengine watasimamia uchaguzi, wengine watashughulika na utawala bora lakini ili wawe halali kwa Tanzania wanalolifanya ni lazima liendane na maadili ya Mtanzania. Hata kama wana cheti, wanachokifanya kisipoendana na maadili ya Watanzania kitakosa uhalali,” amesema Ntimi.

Ofisa Mwandamizi wa Ufuatiliaji na Tathimini wa Ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum , Charles Komba amesema msamaha wa kodi uko kwa mujibu wa sheria ya kodi na hivyo ili kupata msamaha wa kodi kuna utaratibu wake.

“Huko zamani ukisajiliwa kama shirika lisilo la kiserikali maana yake moja kwa moja unapata msamaha, lakini mabadiliko ya sheria yameruhusu mashirika ya kiserikali kuwa na uwezo wa kuwekeza. Kwa hiyo kama unaweza kuelekeza maana yake una mradi ambao unakuletea faida,” amesema.

Kuhusu ada za mwaka, Komba amesema mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani yamekuwa yakilipa Sh50,000 kama ada kwa mwaka, lakini ya nje yamekuwa yakilipa Dola 100za Marekani  kwa mwaka.

“Tuliwasilisha kuwa kuangaliwa kwa namna ambavyo ada haiwezi kuwa flat (sawa) kwa mashirika yote kama ambavyo imetofautisha, mashirika ya ndani na nje basi itofautishe ya watu wenye ulemavu,” amesema.

Amesema jambo hilo ni la kulijadili ili kuangalia namna linavyoweza kutekelezwa, kwa sababu ukigusa tu kwa wenye ulemavu pekee wanaweza kuja na mashirika yanayohusiana na makundi mengine wakitaka afua.

“Ni jambo ambalo la kushirikiana na baraza kutafuta namna nzuri ya kushughulika nalo na pengine ikawa si makundi na kuangalia uwezo wa shirika wa kupata rasilimali. Zipo nchi nyingine unawekewa kiasi fulani cha fedha, kulingana na rasilimali unazoingiza kwa mwaka,” amesema.

Related Posts