Mwinzani: Mtashangaa NCBA, Lugalo Open

CHIPUKIZI wa mchezo wa gofu, Julius Mwinzani wa klabu ya Dar es Salaam Gymkhana, anasema atakuja kuwashangaza wengi katika mashindano ya mchezo huo ya NCBA, Lugalo Open na Lina Tour kwa jinsi alivyopania kama alivyokuwa amejipanga kwa Morogoro.

Mchezaji huyo anayechezea timu ya taifa ya vijana U18, alisema hayo baada ya kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Morogoro Open.

Mwinzani alishika nafasi ya tatu, baada ya kupata mikwaju 233 katika mashindano ya siku tatu yaliyofanyika kwenye viwanja vya Morogoro Gymkhana , huku nafasi ya kwanza ikienda kwa Enoshi Wanyeche kutoka Lugalo aliyeshinda kwa mikwaju 225.

Akizidi kuelezea, alisema  mashindano ya Morogoro Open kwa upande wake yalikuwa ni moja ya kipimo chake kizuri katika mashindano mengine atakayocheza   

“Kwa kweli mashindano hayo yalinisaidia sana kuniweka sawa, ni baada ya kuchuana na wachezaji wazoefu wa timu ya taifa ambao ni Ally Mcharo, George, Sembi na Isihaka Daudi,” alisema Mwinzani.

Akizungumzia kuhusiana na mashindano hayo matatu makubwa, alisema amejipanga vizuri kushinda mashindano ya kwanza ya  NCBA yatakayofanyika Juni  29 kwenye viwanja vya Arusha Gymkhana.

Mengine ni ya Lugalo Gold Open yatafanyika Julai 5-7 kwenye viwanja vya Lugalo, ilihali yale ya Lina Tour ya Juni 11-14 Arusha.

Related Posts