Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mifumo ya kidijitali ya utumishi wa umma itakayoongeza ufanisi katika sekta ya utumishi wa umma huku akiwataka viongozi kuhakikisha usalama wa taarifa ili kuepuka ukiukwaji wa faragha na uhalifu wa kimitandao.
Mifumo hiyo ni Taarifa za Kiutumishi na Mishahara, Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji wa Kazi katika utumishi wa Umma na Mfumo wa Tathimini ya Mahitaji ya Watumishi na Mfumo wa Ushughulikiaji wa Mrejesho kwa Wananchi (E-Mrejesho).
Majaliwa amesema hayo leo Jumapili, Juni 23, 2024 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na uzinduzi wa mifumo ya kidijitali uliofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
“Kila taasisi ya umma ihakikishe usalama wa takwimu na taarifa na mifumo yenyewe inabaki kuwa salama. Natambua mifumo hii inatumia taarifa nyingi na nyeti na hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wa taarifa na mifumo yake ya kidijitali ili kuepuka ukiukwaji wa faragha na uhalifu wa kimtandao,” amesema.
Amewataka watendaji wa taasisi kuhakikisha watumishi wanapata mafunzo ya matumizi sahihi ya mifumo hiyo kwa sababu ni mipya.
Aidha, amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kuweka tarehe ya ukomo wa kila taasisi kujiunga na mfumo huo.
“Bila kuweka ukomo jambo hili halitaisha, kila mmoja atakuwa anakwepa na hasa wale wakwepaji wale ambao hawafanyi kazi zao kwa weledi. Lakini endeleeni kuhamisisha mifumo hiyo. Pia wizara iendelee kufanya maboresho kwa kushirikisha sekta na taasisi husika,” amesema Majaliwa.
Awali, Simbachawene amesema uzinduzi wa mifumo hiyo ni mkakati wa Serikali katika kuboresha huduma, kuondoa kero mbalimbali na rushwa.
“Mifumo hii imeendelea kuleta mageuzi ya utendaji wa umma na imesaidia kutatua kero za watumishi wa umma na kuweka uwazi na uwajibikaji wa watendaji kwa wananchi,” amesema.
Amesema mifumo hiyo imesaidia kubaini mahitaji halisi katika utumishi wa umma na kubaini udanganyifu katika michakato ya mishahara.
Amewaagiza watendaji wakuu wanapaswa kuzingatia mifumo ya ulinzi wa kimtandao na sera za usalama zinawekwa na kusimamiwa ipasavyo.
Amesema mfumo wa taarifa za utumishi wa umma na mishahara unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 na umeunganishwa na mifumo mingine ikiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Ametaja faida za mfumo huo ni kupunguza muda wa kuchakata mishahara kutoka siku 14 hadi dakika 30 na uwezo wa kuwaondoa kazini watumishi waliofikia umri wa kustaafu.
“Mfumo huu umeongeza usahihi wa taarifa na kudhibiti udanganyifu kwa baadhi ya watumishi uliosababisha uwepo wa watumishi hewa,”amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Florent Kyombo amesema wabunge walikuwa ni waathirika wakubwa wanaporudi majimboni kwa kulazimika kuwasaidia watumishi wa umma kufika Dodoma kufuata huduma.
“Tulikuwa tunapokea watumishi wengi hapa Dodoma, lakini leo uhamisho anaufanya akiwa nyumbani kwake, taarifa zake za utumishi anazipata akiwa nyumbani kwake na mkopo pia,”amesema.
Naye Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi amesema ofisi yake inatekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kufanyika kwa maboresho katika mfumo wa upimaji wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza uwajibikaji.
Amesema mfumo huo ni taarifa za watumishi na mishahara ambao umewarahisishia shughuli ya kupima utendaji wa watumishi wa umma walionao ikilinganishwa na mfumo wa zamani.