Lindi. Utafiti ya mwaka 2021/22 umeonesha Mkoa wa Lindi una asilimia 21 ya watoto wenye udumavu na uzito pungufu kwa walio chini ya miaka mitano.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Juni 23, 2024, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Lindi, Juliana Chikoti amesema ili kuondokana na hali hiyo, ametoa rai kwa wananchi mkoani humo kutilia mkazo kilimo cha chakula badala ya mazao ya biashara pekee.
Amesema wakifanya hivyo itawasaidia kukabiliana na tatizo la udumavu na uzito pungufu kwa watoto wao.
“Mtoto anapokuwa na hali ya udumavu, inakuwa ngumu kufundishika shuleni na wakati mwingine inapunguza hata nguvu kazi ya Taifa kutokana na kukosa lishe bora tangu utotoni,” amesema Chikoti.
Amesema Mkoa wa Lindi umepiga hatua kubwa katika kupunguza hali ya udumavu na uzito pungufu, kutoka asilimia 35 mwaka 2015/16 hadi asilimia 21 mwaka 2021/22.
Hivyo, Chikoti amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kujitahidi kulima mazao ya chakula ili kuwa na chakula cha kutosha nyumbani, jambo litakalosaidia kuondoa tatizo hilo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Sokoine Mkoani Lindi, Henry Kagya amesema Serikali inalenga kuhakikisha malezi na makuzi ya mtoto yanapewa kipaumbele ili Taifa liweze kupata kizazi bora.
Akifungua kikao cha tathimini ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi ya Mtoto na Maendeleo ya Awali (PJT) leo Jumapili, Dk Kagya amesema programu hiyo imelenga watoto kuanzia siku sifuri hadi miaka minane.
“Mtoto anatakiwa kula vizuri ili kuweka ubongo wake sawa. Anapokuwa na udumavu, haelewi vizuri na Taifa linakosa nguvu kazi,” amesema Dk Kagya.
Dk Kagya amewataka wazazi kujitahidi kuwalea watoto wao ipasavyo na kuacha tabia ya kuwaachia wajukuu wao kulelewa na bibi zao. “Wazazi wanatakiwa kuwalea watoto wao wenyewe na kuacha tabia ya kuwaachia kinabibi,” amesisitiza.
Naye Navil Nestor amesema watoto wanapopata lishe bora, wanakuwa na afya njema na uelewa mzuri.
“Watoto wa sasa wengi wana akili sana kutokana na wazazi wao kufuata zile siku 1,000 za mtoto kupewa lishe bora inayosaidia kukuza ubongo wake,” amesema Nestor.