Taarifa hiyo imethibitishwa na Gavana wa mkoa huo Sergei Melikov alieeleza kuwa watu wenye silaha walishambulia kwa risasi makanisa mawili ya Kiorthodox, sinagogi na vituo vya polisi katika miji miwili ya Derbent na Makhachkala.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Dagestan imesema kundi la watu wenye silaha walifanya mashambulizi hayo karibu wakati mmoja na kwamba kanisa na sinagogi vyoote viliteketea kwa moto.
Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi nchini Urusi imeyahusisha mashambulizi hayo kuwa vitendo vya kigaidi na kutangaza siku tatu za maombolezo katika mkoa huo wa Dagestan wenye Waislamu wengi.
Soma pia: DAGESTAN : Polisi watatu wauwawa katika mripuko
Mamlaka imetangaza operesheni ya kukabiliana na ugaidi katika eneo hilo na kubainisha kuwa watu watano wenye silaha “walitokomezwa.” Haikuwa wazi ni jinsi gani wala wapiganaji wangapi walihusika katika mashambulizi hayo.
Hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulizi hayo licha ya mamlaka kuanzisha uchunguzi wa makosa ya jinai kwa shtaka la vitendo vya kigaidi.
Watu wanne wauawa na wengine 124 wajeruhiwa katika rasi ya Crimea
Katika tukio jingine, Urusi imesema Marekani imehusika moja kwa moja katika mashambulizi yaliyofanywa na Ukraine katika rasi ya Crimea na kusababisha vifo vya watu 4 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 124. Moscow imeilaumu Washington kwa kuipatia Kyiv makombora ya kisasa yaliyotumiwa katika shambulio hilo.
Soma pia: Ukraine yasema imeshambulia mifumo ya kujilinda angani iliyoko Crimea
Mamlaka za Urusi zimesema watoto wawili ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio la roketi huko Sevastopol katika rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi mnamo mwaka 2014.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewatolea wito washirika wake wa Magharibi kuipatia Kyiv silaha zaidi za kimkakati na kutoa idhini ya kushambulia ndani ya Urusi.
(Vyanzo: APE, DPAE)